![]() |
| Meneja Kitengo cha Utangazaji Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka akiwasilisha mada kwenye mkutano huo. |
Changamoto za Uwekezaji katika Utangazaji Vijijini Zabainishwa.
Changamoto mbalimbali zimeibuliwa kuhusu hali ya uwekezaji katika sekta ya utangazaji vijijini, huku ikielezwa kuwa bado kuna pengo kubwa kati ya maendeleo ya teknolojia mijini na hali ilivyo katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika mjadala kuhusu Hali ya Uwekezaji wa Utangazaji Vijijini, mchangia mada alieleza kuwa licha ya teknolojia kukua kwa kasi katika miji mikubwa, vijijini maendeleo hayo bado ni hafifu. Hali hiyo imechangia kuwepo kwa changamoto nyingi kuliko fursa katika sekta ya habari vijijini.
Imeelezwa kuwa uwekezaji umekuwa ukikwama mara kwa mara kutokana na ukosefu wa wataalamu. Vijana wengi wenye elimu na ujuzi wamekuwa hawako tayari kubaki vijijini, wakihamia mijini wakivutiwa na kasi ya maendeleo na fursa zinazoonekana kuwa nyingi zaidi.
Aidha, changamoto ya nishati ya umeme pamoja na gharama na upatikanaji wa matengenezo ya vifaa vya utangazaji imeelezwa kuwa kikwazo kikubwa. Vilevile, taasisi nyingi zinakabiliwa na tatizo la wafanyakazi kutokubali kupangiwa vituo vya kazi vijijini.
Licha ya ukweli kwamba vijijini kuna maudhui muhimu yanayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa, kasi ya uwekezaji kutoka kwa wadau wa habari bado ipo chini. Takwimu zinaonesha vijana wengi wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanahama vijijini kwenda mijini.
Kwa mfano, takwimu za sensa zinaonesha kuwa Dar es Salaam imeendelea kupokea idadi kubwa ya wahamiaji. Kutoka takribani watu milioni 2 katika sensa ya awali, hadi kufikia zaidi ya milioni 5.3 katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 50 ya vijana wanaohamia jijini humo wanatoka vijijini, wakivutiwa na taswira ya Dar es Salaam kuonekana kama kitovu cha fursa na mafanikio.
![]() |
| Sehemu ya Washiriki katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa vyombo vya Utangazaji (ABC 2026) ulioanza leo tarehe 12 na kutarajiwa kutamatika kesho 13 Februari 2025, Jijini, Dodoma. |
Mapendekezo ya Maboresho
Ili kukabiliana na changamoto hizo, imependekezwa kuwa:
Kila kituo cha utangazaji kiunde mkakati maalum wa kutambua, kuibua na kuanisha fursa zilizopo vijijini.
Vijana wapewe elimu ya kujitambua inayozingatia mazingira halisi ya sasa.
Maboresho ya sera za sekta ya utangazaji yafanyike ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji vijijini.
Miundombinu ya nishati na mawasiliano ya mtandao iboreshwe.
Serikali itoe ruzuku kwa vituo vya habari vinavyofanya kazi vijijini ili kuviwezesha kujiendesha kwa ufanisi.
Imeelezwa kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo unawezekana kwa kuwa jamii sasa imepata uelewa mpana wa aina ya elimu na maendeleo inayoyahitaji.
![]() |
| Sehemu ya Washiriki katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa vyombo vya Utangazaji (ABC 2026) ulioanza leo tarehe 12 na kutarajiwa kutamatika kesho 13 Februari 2025, Jijini, Dodoma. |
Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Utangazaji
Hoja hizo zimejadiliwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji, unaofanyika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka Februari 13.
Kitaifa, maadhimisho hayo yanafanyika katika makao makuu ya nchi, Dodoma, yakiwa na kauli mbiu: “Matumizi ya Teknolojia katika Kupanua na Kuboresha Huduma za Utangazaji Vijijini".

Tupe maoni yako

























0 comments:
Post a Comment