ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, February 13, 2026

SERIKALI YATOA NAFUU KWA WAWEKEZAJI WA MAUDHUI YA HABARI MTANDAONI

 

SERIKALI imechukua hatua ya kihistoria ya kuchochea ukuaji wa sekta ya habari za kidijitali nchini kwa kupunguza kwa kiwango kikubwa ada za leseni kwa wanablogu na wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, hatua inayolenga kuondoa vikwazo vya gharama na kufungua fursa zaidi kwa wabunifu wa maudhui.

Hatua hiyo imetangazwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji (ABC) Februari 12, 2026 jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, ada ya leseni kwa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka Shilingi 1,000,000 hadi Shilingi 100,000 kwa mwaka, huku ada ya fomu ya usajili ikishuka kutoka Shilingi 100,000 hadi Shilingi 20,000.

Aidha, ada ya leseni kwa blogu imepungua kutoka Shilingi 500,000 hadi Shilingi 50,000 kwa mwaka, na fomu ya usajili kushuka kutoka Shilingi 50,000 hadi Shilingi 10,000.


Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri Mwinjuma amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya utafiti wa kina na majadiliano ya kimkakati yaliyodumu kwa takribani mwaka mmoja kati ya Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) na Tanzania Communications Regulatory Authority (TCRA), yakilenga kuondoa changamoto za gharama zilizokuwa zikikwaza ukuaji wa uandishi wa habari za kidijitali nchini.


Katika hatua nyingine, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka, alitangaza msamaha wa ada ya leseni kwa mwaka mmoja kwa waandishi wa habari wanaoanzisha mitandao ya habari watakaotambulika kama “amateur”, ili kuwapa nafasi ya kujitambulisha rasmi na kukuza vipaji vyao bila mzigo wa kifedha.

Awali, mwombaji wa kuanzisha mtandao wa habari alitakiwa kulipa ada ya maombi ya Shilingi 50,000 na ada ya leseni ya Shilingi 500,000 kwa mwaka.

Tangazo hilo limepokelewa kwa furaha kubwa na wamiliki wa mitandao waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili, ambapo baada ya kutangazwa rasmi walishangilia na kupiga makofi kuonyesha kuunga mkono hatua hiyo.


Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni wanachama wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), MOAT, NIBA, Wakongwe RTD, Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania na EACO.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment