ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, January 17, 2020

NYONGO AWAONYA WANAOWASUMBUA WAFANYABIASHARA WA MADINI


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza kwenye mkutano na wadau wa madini katika ukumbi wa Mount Meru jijini Arusha.

Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki akizungumza jambo kwenye mkutano na wadau wa madini mwanzoni kushoto ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo anaefata ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akipewa maelezo na mfanyabiashara wa madini katika soko la madini jijini Arusha.
Balozi wa China nchini Tanzania Wang ke akizungumza kwenye mkutano na wadau wa madini katika ukumbi wa Mount Meru jijini Arusha
Balozi wa China nchini Tanzania akikabidhiwa zawadi kutoka kwa mfanyabiashara wa Madini.
 Baadhi ya Wajumbe walioshiriki katika mkutano wa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo jijini Arusha

NAIBU wa Madini Stanslaus Nyongo akitoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa Madini jijini Arusha, mbele kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula na wapili kutoka kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha Mhandisi Khamis Kamando.
Na Tito Mselem Arusha,

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameonya tabia ya  baadhi ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwakamata wafanyabiashara wa madini wenye vibali na wanaofata Sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali katika shughuli hiyo.

Kauli hiyo ameitoa  Januari 15,  jijini Arusha wakati  akifungua Mkutano wa Mabalozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke pamoja na wadau wa madini uliolenga kujadili fursa za biashara katika sekta ya Madini.

“kumeibuka tabia ya kuwakamata na kuwasumbua wafanyabiashara wa madini ambao wengi wao wanavibali halali vya kumiliki madini hii ni kunyanyasa wafanyabiashara wasio na hatia, tumefungua 
masoko ya madini mikoani ili wafanyabiashara wetu wasinyanyasike”, alisema Nyongo.

Aidha, Nyongo, amewataka Polisi watakao kamata wafanyabiashara wakiwa na madini majumbani mwao, kuhakikisha wanawatumia Maofisa Madini ili kujua kama madini hayo yanavibali kwa kuwa sheria inaruhusu wafanyabiashara kukaa na madini ilimradi wanavibali na wafuate sheria.

Alisema ili kuondoa mkanganyiko huo, Wizara imejipanga kuelimisha wadau wa madini vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu sheria za madini ikiwemo inayoruhusu wafanyabiashara hao kushikilia madini kabla ya 
kuyauza katika masoko ya madini.

Pia, Nyongo aliwasisitiza Mabalozi wa China nchini Tanzania Wang Ke na yule wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki kuendelea kuhamasisha wawekezaji  kuwekeza nchini hususan  kwenye masuala ya uongezaji thamani madini chini ya gramu mbili ambayo yanaruhusiwa kwenda nje ya  nchi bila kuongezwa thamani.

"Kama mnateknolojia ya kuongeza thamani madini haya tunawaalika mje kuwekeza ili tusiyatoe nje bila kuongeza thamani,” alisema Nyongo.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Nyongo, amewahakikishia wawekezaji waliowekeza katika Sekta ya Madini mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuhakikisha anasimamia kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema mchango wa Sekta ya Madini katika pato la taifa bado ni mdogo hivyo ipo haja kuendelea kuyatangaza madini yetu na kushiriki maonyesho mbalimbali ya kimataifa.

Amesema serikali imeamua kutumia balozi zake katika kutangaza madini  yanayopatikana hapa nchini ikiwemo madini adimu ya Tanzanite.

Aidha, katika hatua nyingine Gambo, amewahakikishia wawekezaji kutoka China waliowekeza katika Mkoa wa Arusha, mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuwaahidi kwamba atasimamia kuondoa kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji hao.

Alisema nchi ya Tanzania ina madini mengi lakini mchango wake kwa pato la Taifa ni asilimia 5.07 tofauti na pato la Sekta ya Utalii asilimia 17 na asilimia 25 katika kulingizia Taifa fedha za kigeni.

"Mchango huu hautoshi hivyo tumeamua kutumia mkutano huu ili tuongeze fursa katika madini na kukuza zaidi pato la sekta hii," alisema Gambo.

Kuhusu ukusanyaji wa maduhuli ya serikali Gambo alisema yanatokana na soko la madini Namanga ambapo lilikusanya Shilingi bilioni 1.7 na soko la Arusha limekusanya Shilingi bilioni 34.46 katika kipindi cha Juni 2019 hadi Desemba 2019.

Naye, balozi wa Tanzania Nchini China, Mbelwa Kairuki amewataka wafanyabiashara wa madini nchini kujipanga kwa kutafuta viza mapema ili kushiriki soko la madini nchini china linalotarajiwa kufanyika Novemba 10 hadi 15 mwaka huu.

"China ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu kama mwaka jana 2019 walinunua dhahabu tani 1506 hiki sio kiwango kidogo na hata madini mengine wananunua sana hivyo tujitahidi kuongeza fursa za soko nchini China,” alisema Kairuki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amewataka  Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kukaa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuelimishana kuhusu sheria za madini ili  wawe na namna bora ya pamoja ya kudhibiti utoroshaji wa madini nchini.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.