Aidha, Lukuvi ameagiza maofisa hao waliosimamishwa kazi kutokanyaga katika eneo la ofisi za Jiji mpaka hapo uchunguzi utakapofanyika na maamuzi dhidi ya tuhuma zao yatakapotolewa.
Lukuvi alichukua uamuzi huo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Jiji la Arusha jana kufuatia kuwepo tuhuma nyingi za matapeli ya viwanja kushirikiana na baadhi ya maofisa wa ardhi wasiokuwa waaminifu kufanya utapeli kwa wamiliki halali wa viwanja.
Maafisa ardhi waliosimamishwa kwa tuhuma hizo za kushirikiana na matapeli kudhulumu viwanja kwa wamiliki halali katika jiji la Arusha ni Elizabeth Mollel, Lassen Mjema na Zawadi Mtafikikolo.
Mbali na kusimamishwa kazi kwa watumishi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza maafisa Ardhi wa Jiji la Arusha kuhakikisha matapeli wote wa viwanja wanaoshirikiana na watumishi hao wasipatiwe huduma katika masuala yoyote ya ardhi kufuatia kuonekana kujihusisha na mipango ya utapeli wa viwanja kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha.
Katika ziara yake hiyo ya kushtukiza pamoja na kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley Nyato uwepo wa watumishi wawili Lassen na Zawadi huku Elizabeth akiwa katika likizo ya uzazi, watumishi hao walipotea ghafla ofisini bila taarifa mara baada ya kuelezwa wanahitajika kwa waziri na hata pale walipopigiwa simu za mkononi hazikupatikana.
Kwa mujibu wa Lukuvi, watumishi hao wa sekta ya ardhi katika jiji la Arusha wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na matapeli wa viwanja katika jiji hilo jambo linalotia mashaka utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa maafisa hao wamekuwa na tabia ya kufuatilia kesi zilizopo katika Mabaraza ya Ardhi kwa nia ya kuwasaidia matapeli.
Kufuatia kadhia hiyo, Lukuvi ameagiza kuanzia sasa hati zote za wito wa Mahakama nchini kusainiwa na Afisa Ardhi Mteule au Msajili wa Hati ama Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda na Mwanasheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi lazima afahamishwe uwepo wa kesi husika.
“Kuanzia sasa summons zote zipokelewe na Maafisa Ardhi Wateule, Makamishna au Wasajili wa Hati wa Kanda na watumishi wengine wasipokee wala kujihusisha” alisema Lukuvi
Lukuvi alisema matapeli wa viwanja wamekuwa wakifungua kesi katika Mabaraza ya Ardhi dhidi ya wamiliki halali na wakati mwingine matapeli hao hawawafahamu hata wamiliki lengo lao likiwa kuwakatisha tamaa pale kesi inapochukua muda mrefu hasa ikizingatiwa baadhi ya wamiliki hawana uwezo wa kuweka mawakili na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao.
Alisema, tabia hiyo haiwezi kuvumiliwa na kusisitiza kuwa mtandao wote wa matapeli wa viwanja katika jiji la Arusha ataukomesha kama alivyofanya katika jiji la Dar es Salaam ambalo huko nyuma lilishamiri sana kwa tabia hiyo ili kusaidia haki za wanyonge.
Kwa upande wake Afisa Ardhi Mteule wa Jiji la Arusha Dicley Nyato alimueleza waziri Lukuvi kuwa wamekuwa wakisumbuliwa sana na matapeli wa viwanja katika jiji hilo na wakati mwingine matapeli hao huwashitaki lengo likiwa kujipatia viwanja kwa njia ya udanganyifu na kuviuza.
Lukuvi alifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika ofisi za jiji Arusha akitokea wilayani Babati mkoa wa Manyara ambako huko aliweza kutoa faraja iliyopotea kwa muda mrefu kwa wananchi wa vijiji vya Singu na Endasago kwa kuamuru kubaki katika maeneo yao kufuatia mgogoro wa muda mrefu wa takriban miaka hamsini kati ya wana kijiji na wamiliki wa mashamba ambao ni kampuni za Agric Tanzania Ltd na Endasago Co Ltd.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.