ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, April 3, 2018

MHE BITEKO AANZA KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI MKUU LA KUKOMESHA UTORO MASHULENI, ACHANGIA MATOFALI 10,000 UJENZI WA MAABARA

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua majengo ya maabara za shule ya sekondari ya Kata ya Busonzo katika Kijiji cha Nampalahala akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Bukombe, Leo 2 Aprili 2018. Picha Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Kata ya Busonzo katika Kijiji cha Nampalahala, Leo 2 Aprili 2018. 
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nampalahala, Kata ya Busonzo wakifatilia mkutano wa hadhara ukiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Bukombe, Leo 2 Aprili 2018.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nampalahala, Kata ya Busonzo wakati akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Bukombe, Leo 2 Aprili 2018.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua ujenzi wa nyumba za madaktari wa kituo cha afya cha Uyovu akiwa katika ziara ya siku moja Wilayani Bukombe, Leo 2 Aprili 2018.

Na Mathias Canal, Geita

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko Leo 2 Aprili 2018 amechangia matofali 10,000  kwa ajili ya ukamilishaji Wa vyumba vya maabara ili kurahisisha uanzisha Wa shule ya sekondari Kata ya Busonzo Wilayani Bukombe.

Shule ya sekondari Busonzo inahitaji kukamilisha maabara tatu ili iweze kufunguliwa ambapo serikali imetoa milioni 40 kwa ajili ya kazi hiyo.

Mhe Biteko amechangia matofali hayo Mara baada ya maagizo ya Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa aliyoyatoa wakati Wa dhifa ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja wa Magogo mkoani Geita kwa kuwataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za msingi na kwa sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.

"Mkoa wetu tumepata aibu kubwa kwa kuwa namba mbili kwa utoro kati ya mikoa yote nchini, utoro huu hapa wilayani kwetu unachangiwa na umbali wa kwenda shuleni, hapa Busonzo watoto wetu wanasoma Runzewe ambapo ni mbali sana. Umbali huo unachangia utoro" alisisitiza Mhe. Biteko

Katika sherehe hizo zilizonakshiwa na Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ambayo ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’ Waziri Mkuu alisema kuwa utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa Mikoa husika kuliko shule za msingi. 

Mara baada ya uzinduzi Wa Mwenge huo wa Uhuru kabla ya kuelekea Mjini Dodoma kwa ajili ya shughuli za Bunge zinazotarajiwa kuanza kesho 3 Aprili 2018 Mhe Doto Biteko amezuru Kijiji cha Nampalahala kilichopo Kata ya Busonzo na kujionea jinsi ujenzi Wa maabara unavyoendelea.

Mara baada ya kubaini kuwa kuna upungufu wa matofali 10,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo, Naibu Waziri huyo amechagiza ujenzi huo kwa kuchangia gharama za ununuzi wa matofali hayo ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

"Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo ya kukomesha utoro naomba tukimbie kulitekeleza hilo na ninaomba wazazi tuhakikishe watoto wote wanakuwa shuleni ni aibu mno sisi kuwa vinara wa utoro". Aliongeza Mhe. Mbunge Na Naibu Waziri huyo.

Mhe Biteko amewaeleza wananchi hao jinsi ambavyo utoro kwa shule za sekondari Mkoani Geita umekithiri jambo ambalo limepelekea Mkoa huo kushika nafasi ya pili kwa utoro Kitaifa kwa asilimia 8.1, ambapo Mtwara imekuwa nafasi ya tatu kwa asilimia 6.4, Shinyanga asilimia 6.3 huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Mkoa Wa Tabora kwa asilimia 9.7 

Aidha, Mhe Biteko ameonyesha kusikitishwa na takwimu za Mkoa Wa Geita kushika nafasi ya pili pia katika kwa utoro kwa shule za msingi kwa kwa asilimia 3.1 nyuma ya Mkoa Wa Rukwa unaoongoza kwa asilimia 3.2

Aliongeza kuwa anatamani kuona  Wilaya ya Bukombe inahakikisha inafikia viwango bora vya elimu. Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa maendeleo ya wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla aliwaomba pia wananchi wa  kata ya Busonzo kumuombea Rais Magufuli na kuunga mkono juhudi za serikali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.