Na. Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi
nchini limesema Operesheni ya kukabiliana na mtandao wa dawa za kulevya katika
Visiwa vya Zanzibar itaendelea sambamba na kuwadhibiti wahalifu wanaofanya
vitendo vya kuwaibia na kuwadhuru watalii jambo ambalo linatia doa usalama
uliopo katika visiwa hivyo.
Kauli hiyo
imetolewa na Mkuu wa Operesheni maalum
za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Liberatus Sabas ambaye yupo Zanzibar
akiongoza timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na Kamisheni
ya Polisi Zanzibar kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuzuia na kupambana na
mtandao wa dawa za kulevya pamoja na uhalifu dhidi ya watalii.
DCP Sabas amesema
Operesheni hiyo haitawaacha wahalifu hao salama kwa kuwa inafanyika kwa umakini
mkubwa ili kuhakikisha kuwa haiachi mhalifu yeyote anayejihusisha na vitendo
hivyo viovu ambavyo vimekuwa vikichafua taswira nzuri ya usalama.
“Operesheni hii ni
endelevu na niwape tu salamu wahalifu kuwa jambo la msingi ni wao wenyewe kujisalimisha
kwa kuwa awamu hii hata wakikimbia tutawasaka na kuwakamata kwa kuwa nguvu ipo na tunapata ushirikiano
kwa wananchi wema wanaochukia vitendo vya uhalifu” Alisema Sabas.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa
Polisi Hasina Tawfiqi amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya Heroin jumla ya Kete 695 sawa na
ujazo wa gramu 31.3 pamoja na Watuhumiwa 21.
Amewasihii wakazi wa Kaskazini Unguja na mikoa jirani
kuendelea kutoa taarifa ili kuweza kukomesha mtandao wa biashara hiyo pamoja na
kuhakikisha kuwa watalii wanaotembelea mkoa huo wanafanya kazi zao kwa amani na
usalama.
Operesheni hiyo pia imefanyika katika Mkoa wa
Mjini magharibi ambapo Jumla ya watuhumiwa 58 walikamatwa pamoja na dawa za
kulevya aina heroin Kete 1293 na Vifuko vitatu sawa na Gramu 74.385.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.