ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, January 13, 2018

KOMBE LABAKI NYUMBANI TANZANIA - NI AZAM FC TENA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI.



Na Salum Vuai, ZANZIBAR
AZAM FC imetwaa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya pili mfululizo baada ya ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya URA ya Uganda kufatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, shujaa wa Azam FC alikuwa ni mlinda mlango, Mghana Razack Abalora aliyecheza penalti mbili za wachezaji wa URA.

Abalora aliye katika msimu wake wa kwanza Azam FC tangu asajiliwe kutoka West African Football Academy (WAFA FC) ya Ghana alipangu penalty ya kwanza ya URA iliyopigwa na Parrick Mbowa nay a mwisho iliyopigwa na Brian Majwega.


Waliofunga penalti za Azam FC ni Nahodha Himid Mao, Yakubu Mohammed, Enock Atta Agyei na Aggrey Morris wakati Bruce Kangwa alimpelekea mikononi mpira kipa wa URA, Alionzi Nafian na penalti za URA zimefungwa na Charles Ssempa, Shafiq Kagimu na Jimmy Kulaba.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa mkongwe visiwani hapa, Mfaume Nassor aliyesaidiwa na Mbaraka Haule na Dalila Jaffar, dakika 90 zilikuwa ngumu timu zote zikishambuliana kwa zamu na ziwaendee makipa wa timu zote, Abalora na Alionzi Nafian kwa kuokoa vizuri.

Ushindi huu unamaanisha Azam FC wanatwaa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya nne ya rekodi, baada ya awali kulibeba pia katika miaka ya 2012, 2013 na 2017 wakiipiku Simba SC ya Dar es Salaam iliyotwaa mara tatu 2008, 2011 na 2015. 
    
Yanga SC ndiye bingwa wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2007 wakati timu nyingine zilizotwaa taji hilo ni Miembeni mwaka 2009, Mtibwa Sugar mwaka 2010 na KCCA ya Uganda mwaka 2014.

Jumla ya timu 11 zilishiriki michuano ya mwaka huu ambazo ni URA, Jamhuri, Mwenge, Azam na Simba zilizokuwa Kundi A na Zimamoto, Mlandege, Yanga, JKU, Taifa Jan’gombe na Singida United zilizokuwa Kundi B.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Abdallah Kheri/Joseph Mahundi dk59, Stephan Kingue, Frank Domayo/Iddi Kipagwile dk58, Salmin Hoza, Bernard Arthur/Shaaban Iddi dk58 na Yahya Zayed/Enock Atta-Agyei dk64.

URA;Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan Munaaba, Patrick Mbowa, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba, Kalama Deboss/Charles Ssempa dk66, Moses Sseruyide/Peter Lwasa dk81, Hudu Mulikyi na Shafiq Kagimu/Jimmy Kulaba dk82.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.