Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akifungua rasmi migodi ya Buhemba ya wachimbaji wadogo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akishuhudia tukio hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akizungumza wakati wa ufunguzi wa migodi ya wachimbaji wadogo ya Buhemba, Mkoani Mara.
MGODI WA BUHEMBA WAFUNGULIWA RASMI
Hatimaye Serikali imefungua Migodi ya
Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo iliyopo katika eneo la Buhemba Wilaya ya Butiama
Mkoani Mara baada ya kujiridhisha hali ya usalama katika migodi hiyo.
Migodi hiyo imefunguliwa rasmi na
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Januari 13, 2018 na kushuhudiwa na
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose
Nyamubi.
Akizungumza katika tukio hilo, Nyongo
alisema jumla ya migodi 10 imefunguliwa kati ya 16 baada ya kujiridhisha
usalama wake.
Alifafanua kwamba eneo la Buhemba
lina jumla ya Migodi ya Dhahabu 16 ambayo inamilikiwa na Wachimbaji Wadogo hata
hivyo iliyokidhi vigezo vya kiusalama ni Migodi 10 pekee ambayo imeruhusiwa
kuendeleza shughuli za uchimbaji.
Alisema Serikali ilisitisha shughuli
za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea
vifo vya Wachimbaji Saba na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya
shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.
Alibainisha kuwa Mwezi Desemba mwaka
jana alifanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo
husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli
zao ambapo aliagiza shughuli za ukaguzi zikamilike ifikapo Mwezi huu wa Januari
ili migodi ifunguliwe.
"Kama mtakumbuka nilifanya ziara
hapa na niliagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la
Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji
zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe; tumejiridhisha mashimo kumi ni salama na
sasa tunafungua rasmi," alisema Naibu Waziri Nyongo.
Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi kama
alivyokua ameagiza ilifanyika kwa umakini na kwamba maduara Kumi (Migodi Kumi)
yameruhusiwa na mengine Sita hayatoruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.
Aliongeza kuwa baada ya kufika kwenye
eneo hilo kwa mara ya kwanza alisikitishwa kuona wananchi wengi wakiwa wamekosa
shughuli za kufanya kutokana na migodi hiyo kufungwa na ndiyo sababu ya kuagiza
ukaguzi wake ukamilike haraka.
“Nilivyotembelea hapa Mwezi Desemba
mwaka jana nilisikitishwa kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba
zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea
ajali,” alisema.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwaagiza
Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya migodi ili
kukagua hali ya usalama pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji salama kwa
wachimbaji hususan wadogo lengo likiwa ni kuepusha ajali.
“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi
wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha
ajali,” aliagiza Naibu Waziri.
Naibu Waziri Nyongo vilevile
aliwaagiza wachimbaji madini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu
za uchimbaji ili kuepusha ajali migodini na wakati huohuo kunufaika ipasavyo na
shughuli zao bila kupata usumbufu.
Aidha, Naibu Waziri alizungumzia
ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali ambapo aliwaagiza wachimbaji hao kuhakikisha
wanalipa kwa mujibu wa sheria na alionya kwamba mgodi utakaoshindwa kulipa
inavyostahili, utafungiwa.
"Tumewafungulieni migodi yenu
tukiamini kwamba nanyi mtatimiza wajibu wenu wa kulipa kodi kwa mujibu wa
sheria. Mkishindwa kulipa, hatutosita kuifungia," alibainisha Nyongo.
Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara
kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa migodi na kuzungumza na wachimbaji wadogo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.