Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini (hawapo pichani) alipokuwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) akimsikiliza Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (kulia aliyesimama) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini (hawapo pichani) alipokuwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Mtinika (aliyesimama) akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa tatu kushoto waliokaa) ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akiagana na Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (kulia) mara baada ya kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Mkoani Mbeya. Kushoto ni Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Benedict Bahati.
MKANDARASI
WA REA KUCHUKULIWA HATUA
Shirika la Umeme
Tanzania limeagizwa kumchukulia hatua Mkandarasi ambaye ni kampuni ya wazawa ya
JV State Grid Electrical & Technical Works Ltd aliyekuwa akitekeleza Mradi
wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) Mikoa ya Mbeya na Songwe kwa kushindwa
kukamilisha katika baadhi ya maeneo kwa mujibu wa makubaliano.
Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu ametoa agizo hilo Januari 5, 2018 kwenye mkutano na
wananchi wa Kijiji cha Utengule Usongwe, Mbeya Vijijini alipokuwa kwenye ziara
ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Umeme Vijijini.
Mgalu alitoa agizo
hilo kufuatia taarifa ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Benedict
Bahati ambaye alimueleza kuhusu kampuni hiyo iliyokuwa ikitekeleza Miradi
katika Wilaya za Mbarali, Rungwe, Kyela na Ileje kushindwa kukamilisha miradi
yake kama ilivyopaswa kulingana na mkataba.
Alisema Serikali
haitowafumbia macho Wakandarasi walioshindwa kukamilisha utekelezaji wa Miradi
waliyokabidhiwa kwa mujibu wa makubaliano na aliliagiza Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha Mkandarasi
huyo anapatikana na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa
makubaliano ya awali.
“Serikali
haijaribiwi, tutachukua hatua kwa Wakandarasi wote walioshindwa kutekeleza Miradi
waliyokabidhiwa kwa mujibu wa Sheria; TANESCO na REA, hakikisheni Mkandarasi
huyu anapatikana na hatua stahiki za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,”
alisema Mgalu.
Mgalu aliagiza Mkandarasi
huyo apatikane ndani ya Siku Saba ili aeleze sababu za kushindwa kutekeleza
mradi huo kwa kiwango kilichokubaliwa na kwa muda wa makubaliano. “Nataka ndani
ya Siku Saba tukutane nae aeleze kwanini hajakamilisha mradi kwa mujibu wa
mkataba wake,” alisema.
Aliongeza kuwa
Serikali imedhamiria kuwainua Wakandarasi wazawa hata hivyo katika utekelezaji
wa miradi hiyo ya REA, imedhihirika kwamba walio wengi wameshindwa kutekeleza
miradi waliyokabidhiwa kwa mujibu wa makubaliano.
Aidha, Naibu Waziri
Mgalu alionya Wakandarasi waliopewa jukumu la kutekeleza Miradi ya Umeme
Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuhakikisha wanatekeleza kwa mujibu wa mkataba
na kwamba Serikali haitomvumilia Mkandarasi atakayekwenda kinyume.
“Wakandarasi mnaotekeleza
mradi wa REA III; anayeona hawezi kazi atupishe; hatutomvumilia Mkandarasi anayeharibu
kazi,” alionya Naibu Waziri Mgalu.
Alisema dhamira ya
Serikali ni kuhakikisha Miradi ya Umeme Vijijini inakamilika kwa kiwango
kinachokubalika na kwa wakati kama inavyoelekezwa kwenye mikataba waliyoingia
na Serikali.
Naibu Waziri Mgalu
yupo Mkoani Mbeya kwa ziara ya kukagua na kujiridhisha utekelezaji wa Miradi ya
Umeme Vijijini hususan ya REA pamoja na kuzungumza na Wananchi na Wakandarasi kuhusiana
na utekelezaji wake.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.