ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, July 27, 2017

DK. KIGWANGALLA AKABIDHI GARI LA WAGONJWA JIMBONI KWAKE


Gari hilo la kubebea wagonjwa linavyoonekana

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, Mh. Geofrey Ngupula akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa gari jipya na la kisasa la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa katika kituo cha Afya Busondo, Tarafa ya Puge, lililotolewa na Mbunge wa Nzega Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla.



Mkuu wa Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, Mh. Geofrey Ngupula akizungumza mara baada ya kuzindua rasmi gari jipya na la kisasa la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa katika kituo cha Afya Busondo, Tarafa ya Puge, lililotolewa na Mbunge wa Nzega Vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mbunge wa jimbo la Nzega Vijijini ambaye pia ni Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla amekabidhi gari maalum la kubebea wagonjwa (Ambulance) mpya na la kisasa katika Kituo cha Afya Busondo kilichopo Tarafa ya Puge ambalo litakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Nzega Vijijini.

Tukio hilo la kukabidhi gari hilo limefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, mkoani  Tabora, Mh. Geofrey Ngupula mapema Julai 26,2017, aliyekuwa mgeni rasmi ambaye alitoa agizo kali kwa Mganga Mkuu wa Kituo hicho kuhakikisha gari hilo linatumika kwa shughuli zilizokusudiwa ikiwemo za kubebea wagonjwa na akina mama wajawazito kuwawaisha sehemu muhimu za kutolea huduma stahiki.

Mkuu wa Wilaya huyo alimpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Dk. Kigwangalla kwa kuweza kuwasaidia wananchi  wa Jimbo hilo kwa kuweza kuwasaidia gari hilo la Wagonjwa  kwani litasaidia kuokoa maisha ya wananchi hao ambao wapo maeneo ya mbali na kituo cha Afya huku pia likitarajiwa kuwa msaada kwa kuwapeleka wateja katika  ngazi za juu za huduma hiyo ikiwemo Hospitali za  Wilaya, Mkoa, Kanda na Taifa.

Aidha, alisema ni marufuku wagonjwa kuombwa  kuchangia mafuta ya  ambulance hiyo au gharama yoyote ile, gari hili wagonjwa walitumie bure kwani limetolewa bure na pia huduma zote zikiwemo za mafuta zinalipwa na Halmashahuri hiyo.

“Gari hilo lipatikane kituoni  wakati wote pamoja na dereva. Tumeshahakikishiwa hapa Halmshauri imesema ina mafuta ya kutosha litakuwa linajazwa lita 90, kila yatakapokuwa yametumika hivyo kusiwe na kisingizio kingine cha kuweza kudai mafuta ama kuwatoza wananchi gharama na atakayefanya hivyo Serikali hii si ya mchezo hatua kali zitafuata , tutakutumbua tu” alieleza Mh. Ngupula.

Ameongeza kuwa gari hilo ambalo ni la kisasa, litunzwe na kulindwa ili liweze kutumika kwa miaka mingi ijayo na kuwa  msaada kwa Tarafa hiyo na wananchi wote watakaopata msaada wakiwemo wale wa maeneo mengine ya jirani.

Kwa upande wake, Dk. Kigwangalla amewaomba wananchi waendelee kumuombea kwa kazi anayofanya ikiwemo jukumu la kulitumikia Taifa katika nafasi yake ya Unaibu Uwaziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Dk. Kigwangalla ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli  kwa kuweza kuwa karibu na Wananchi ikiwemo kushughulikia suala la maji kutoka Ziwa Victoria na kuja Mkoa wa Tabora ikiwemo kuanzia katika Wilaya hiyo ya Nzega na kisha kwenda maeneeo mengine.

“Tunampongeza Rais wetru Dk. Magufuli kwa kuwa karibu na wananchi wake. Tulikuwa nae Mkoani kwetu hapa Tabora na amezindua miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara na ule wa maji safi yatakayotoka Ziwa Vitoria. Shida ya maji kwa wananchi wa Nzega inaenda kuwa historia kwani Maji hayo yatakuja hapa na kisha kwenda maeneo mengine. Rais wetu anatupenda na tuendelee kumuunga mkono hasa juhudi zake za kulinda rasilimali za nchi yetu na pia katika kushughulikia mafisadi na wahujumu uchumi wa Taifa letu

Mimi Mbunge wenu pia muendelee kuniombea na kila siku mawazo yangu na akili yangu ipo pamoja nanyi ndio maana nimeweza kuwaletea gari hili la wagonjwa, na pia kufanikisha kuandaa kambi maalum ya matibabu bure ya wiki moja kwa wananchi wote wa Nzega bure inayoendeshwa na Madaktari bingwa wakiwemo wale wa kutoka China na waliopo hapa nchini” alieleza Dk. Kigwangalla.

Tukio hilo la ukabidhi wa gari hilo pia lilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Jimbo hilo na wale wa jimbo jirani ikiwemo Bukuene, Viongozi wa ulinzi na Usalama pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nzega.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.