Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti juzi na jana katika mikoa ya Singida na Morogoro. Waziri Mwigulu Akihutubia wananchi katika Kijiji cha Kaselya wilayani Iramba, Singida juzi katika siku ya kwanza ya ziara ya siku tatu kutembelea jimbo lake, Mwigulu alisema anahusisha mauaji hayo na siasa kwa kuwa mauaji ya wananchi kwenye maeneo hayo yanawakumba zaidi wafuasi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alihoji; “Ujambazi gani huo wa Wana CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.” Alisema wanaodhani kuwa upinzani ni kwenye maisha wanakosea. “Naomba tupingane kwa kushindanisha sera na wala tusikunjiane ngumi kwa ajili ya siasa kwa kuwa siasa haipaswi kuwa ya uadui,” alisema.
Alisema pamoja na siasa hazipaswi kuwa ya uadui bado wapo baadhi ya wapinzani wanaotengeneza siasa ili zionekane kuwa ni za uadui. “Watu hawa wangekuwepo wakati wa vita baina ya nchi yetu na Uganda, hakika wangemsaidia Iddi Amin; bahati nzuri walikuwa bado wadogo,” alisema Waziri.
Sirro na uzalendo Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Sirro amevitaka vyombo vya habari nchini kuwa na uzalendo ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa taarifa zenye kuchochea hofu kwa wananchi.
Alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro ambapo alisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitumia maneno yanayoongeza hofu kwa wananchi.Kuhusu mauaji yanayotokea katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, alisema vyombo vya dola vinaendelea kuyadhibiti na kwamba, jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za kuchochea hofu.
“Taarifa zinazotolewa kwa umma hazioneshi kama kuna kazi inafanyika na vyombo vya dola kuzima mauaji hayo,” alisema Aidha, alisema pamoja na habari hizo kujenga hofu kwa jamii, pia zimekuwa zikiambatana na picha za watu waliojeruhiwa, picha za silaha kuonesha Pwani ni eneo la vita.
IGP Sirro aliwataka wanahabari wanapoandika masuala ya kiusalama, watafute ufafanuzi kwenye vyombo husika ili waandike taarifa sahihi, ikiwa ni pamoja na kutanguliza uzalendo mbele huku wakitambua athari zinazotokana na taarifa hizo kwa jamii.
Alisema wananchi wakijawa na hofu, watashindwa kutekeleza shughuli zao za kijamii na kiuchumi. “Epukeni sana kuandika habari zenye sura ya kishabiki kwenye suala hili, habari nyingi mnazoandika kwenye suala hili mnaonesha kama vile mnalifurahia, hili si suala la kufurahia hata kidogo,” alisema Alisema hayo ni mapambano hivyo kila mmoja anawajibika katika kusaidia ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuzuia uhalifu na kuwakamata wahalifu.
Mkuu huyo alitaka wananchi kushirikiana na na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya dola ili kuwezesha nchi kuendelea kuwa yenye amani na utulivu Aidha, alisema hadi sasa kuna baadhi ya watuhumiwa wameshakamatwa na kwamba upelelezi sio suala la mara moja hivyo, jamii inapaswa kuwapa muda.
“Niwahakikishie wananchi kwamba vyombo vya dola vinafanya kazi kubwa usiku na mchana kuhakikisha tunazima mauaji hayo yanayotokea katika baadhi ya maeneo ya Pwani,” alisisitiza. Aidha aliwataka askari kuwa wa kwanza katika suala la nidhamu na weledi ikiwa ni pamoja na kutii sheria bila shuruti.
Alisisitiza kuwa, askari atakayekiuka maadili ya kazi sheria, achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria zao. “Haiwezekani askari unamkamata mtu hajavaa helmeti wakati wewe mwenyewe hujavaa,” alisema Aidha aliwataka askari wao kuwa wa kwanza na mfano bora katika utekelezaji wa sheria bila shuruti. Imeandikwa na Agnes Haule, Morogoro na Abby Nkungu, Iramba CHANZO: HABARI LEO.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.