KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba ataingia kwenye mchezo wa kesho dhidi ya mahasimu, Simba hali ya kikosi chake ikiwa si nzuri sana.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports - Online leo, Lwandamina amesema kwamba wachezaji wake wanne tegemeo wote ni majeruhi na hawawezi kucheza kesho.
Lwandamina aliwataja wachezaji majeruhi ni Wazambia wenzake, viungo Justin Zulu na Obrey Chirwa na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
Pamoja na hao, Lwandamina alisema beki Pato Ngonyani na mshambuliaji Matheo Anthony nao wote ni wagonjwa na hawana uhakika wa kucheza kesho.
Kwa ujumla Lwandamina ambaye timu yake ilifungwa 4-0 na Azam FC Jumamosi kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi A, alisema ataingia kwenye mchezo wa kesho katika mazingira magumu ya kukatisha tamaa.
“Lakini hatuna namna nyingine, lazima tuingize timu tukapambane,”alisema. Yanga inakutana na mahasimu, Simba katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.