WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara (Mb.) ametuma salamu za rambirambi kwa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA) na Waislamu wote nchini kufuatia kifo cha Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba kilichotokea Jumatatu, tarehe Juni 15,2015 katika hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam alipokuwa anatibiwa.
Katika salamu hizo, Mhe. Mukangara amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kumpoteza kiongozi huyo ambaye bado Taifa lilikuwa likimuhitaji hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Waziri huyo ameongeza kuwa Mufti atakumbukwa kwa upole, unyenyekevu wake na kutopenda makuu,wakati wa uhai wake marehemu alikuwa tayari kumsikiliza kila mtu bila kujali dini au kabila lake.
“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya kifo cha Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba ambaye alikuwa Kiongozi anayeshirikiana vizuri na viongozi wote wa serikali na vyama mbalimbali katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa wamoja” amesema .
Amesema Waziri Mukangara: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi wewe Katibu Mkuu, BAKWATA na waislamu wote nchini na naungana nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu.
Aidha, kupitia BAKWATA, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu kwa kumpoteza mpendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke pema peponi roho ya marehemu … Amina.”
Imetolewa na;
Idara ya Habari(MAELEZO)
WAKATI HUO HUO.
Na Chalila Kibuda.
MWILI wa Mufti ,Alhaj Sheikh Shaban Issa Bin Simba unatarajiwa kusafirishwa kesho mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata),Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam,Alhaj Mussa Salum amesema mwili wa marehemu utaswaliwa kesho katika Msikiti wa Msilimu ,viongozi mbalimbali wa dini na serikali watakuwepo.
Amesema marehemU alikuwa akisumbuliwa na sukari,Shinikizo la Damu (BP) pamoja na Figo.
Hata hivyo amesema kuwa jana (Jumapili) Mufti alifanyiwa oparesheni ya figo katika Hospitali ya TM Jijini Dar es Salaam na Mauti ya Mufti yamekuta majira ya saa moja leo.
Salum amesema marehem anatarajiwa kuzikwa Alhamis mkoani Shinyanga.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.