ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, June 15, 2015

CCM MKOA WA MWANZA YATOA RAI KWA VYAMA VYA SIASA KUACHA KAMPENI ZOEZI LA UANDIKISHAJI

Katibu Mwenezi wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza, Saimon Mangelepa.
NA PETER FABIAN, MWANZA.

HALMASHAURI kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, imeviasa vyama vya siasa kutofanya kampeni wakati vinapopita kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura katika maeneo mbalimbali mkoani Mwanza.

Hayo yamesemwa kwa waandishi wa habari juzi na Katibu Mwenezi wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza, Saimon Mangelepa, kuwa Kikao cha Halmashauri kilichoketi na kupitia ajenda zake kimeazimia kutoa rai kwa vyama vya siasa kuacha kuvuruga zoezi la uandikishaji kwenye vituo kwa kuendesha kampeni zisizo rasmi na zilizo kinyume na maelekezo ya Tume.

Mangelepa alisema kwamba kumekuwa na taarifa za baadhi ya viongozi na wafuasi wa vyama vya siasa wamekuwa wakipita kwenye vituo na ajenda zao za kuvuruga zoezi la uandikishaji kwa kuwahamasisha wananchi kutovipigia kura baadhi ya vyama vya siasa jambo ambalo ni kinyume na maelekezo na sheria za Tume ya Uchaguzi (NEC).

“Tumejadili taarifa ya hali hiyo iliyoanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya mitaa na Kata katika Wilaya za mkoani hapa ambazo zoezi hilo linaendelea , pia  wajumbe wa kikao hicho kwa kauli moja imeonya na kuviaasa vyama vya siasa kutofanya kampeni kuwa zinalengo la kuvuruga zoezi hilo lisifanikiwe,”alisema.

Aidha Halmashauli kupitia kikao hicho kimewataka wananchi katika maeneo mbalimbali kuacha kudanganywa na kujiandikisha mara mbili jambo ambalo wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria na kuweza kukumbwa na adhabu ya kifungo cha zaidi ya miaka zaidi ya miwili kama ambavyo kwenye maeneo ya mikoa mingine walibainika na kufungwa jela.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, alisema kwamba kumeibuka matukio na malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwalalamikia waandikishaji wa Tume (NEC) kuwa chanzo cha kuvuruga zoezi kwa kudaiwa kupokea hongo (Rushwa) na kuwaandikisha watu ambao hufika wakiwa wamechelewa na kupewa kipaumbele.

Mtaturu alisema kuwa tayari wamewasilisha taarifa za malalamiko hayo ya wananchi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakuu wa Wilaya na wakurugenzi ili kufatilia kwa ukaribu zoezi hilo na kuwachukulia hatua watakao bainika kufanya mambo kinyume na maelekezo ya NEC jambo ambalo linaweza kuleta uvunjifu wa amani.

“Waandikishaji wameanza mchezo mchafu wa kuvuruga utaratibu uliowekwa na tume, lakini pia kuna baadhi ya wenyeviti wa mitaa nao wamelalamikiwa kwa kuwapendelea baadhi ya wafuasi wa vyama vyao vya siasa kwa kuwapa kipaumbele jambo ambalo limetakiwa kuachwa ili kutoleta asira kwa wananchi,”alisisitiza.

Katibu Mtaturu alisema kwamba kikao hicho cha Halmashauri kuu ya Mkoa imewataka Wakurugenzi ambao ni wasaidizi wa Tume kuhakikisha wanasimamia zoezi la uandikishaji hadi wananchi wote wenye sifa wanapata fursa ya kujiandiksha kabla ya kuondoa mashine za uandikishaji za BVR ili kutoleta usumbufu wa kurudi tena eneo moja.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.