ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, October 30, 2014

ASKARI POLISI AMKATA VIDOLE VINNE MFANYAKAZI WAKE KWA PANGA AKIMTUHUMU KWA KUMWIBIA DEKI YA VIDEO.

Steven Magessa (18) akizungumza nasi kusimulia kisa na mkasa.

ASKARI POLISI ASHIKIRIWA KWA KUMKATA MFANYAKAZI WAKE VIDOLE VINNE KWA PANGA KWA MADAI YA KUMWIBIA DEKI YA VIDEO NYUMBANI KWAKE. 

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia askari wake WP Fatuma wa Kituo cha Polisi Igogo wilayani Nyamagana kwa kosa la kumjeruhi mtumishi wake wa ndani kwa mkumkata vidole vyake vinne vya mkono wa kulia kwa panga, akimtuhumu kumwibia Deki ya Video nyumbani kwake. 

Tukio hilo la kujeruhiwa kijana Steven Magessa (18), lilitokea Oktoba 20 mwaka huu katika kijiji cha  Magange Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara nyumbani kwao kijana huyo aliyekuwa amekimbilia huko baada ya kudaiwa kumwibia mwajili wake nyumbani eneo la Igogo.

Akizungumza na G.SENGO BLOG kijana huyo alieleza kuwa kufanya kazi kwa askari huyo kulikuja mara baada ya askari huyo kumfuata kijijini na kumuomba ridhaa ya wazazi wa kijana huyo kuambatana naye jijini Mwanza ili kumsaidia kazi za nyumbani ambapo walikubaliana malipo ya kiasi cha Sh 50,000/= kila mwezi jambo ambalo askari huyo alilikiuka na kushindwa kulitekeleza kwa muda wa miezi sita bila kumlipa mshahara.

“Nilipoona hajanilipa mshahara wangu kwa muda wa miezi sita huku kila ni kimwambia ananijia juu na kunitukana matusi basi nilimuomba ruhusa ya kwenda kijijini Oktoba 15 mwaka huu kumuona mama yangu mzazi aliyekuwa anaumwa ili kupata nafasi ya kurudi nyumbani” alisema.

Ni kidole gumba tu kilicho nusurika kukatwa nacho ilikuwa ni kama bahatikusalia kwani kilikwanyuliwa huku vingine vinne vikifyekwa na panga mkono wa kulia wa Steven Magessa.
Steven alieleza kuwa wakati akiwa kijijini askari huyo (Mwajili wake) alikuwa akimpigia simu kumtaka arudi Mwanza kuendelea na kazi na kudai kuwa atamlipa malimbikizo ya mshahara wake kiasi cha Sh 300,000/= zilizokuwa kama deni, Steven alikubali ombi hilo kwa kuomba atumiwe nauli na pesa kidogo ya kumwachia mama yake, jambo ambalo askari huyo alikaa kimya bila majibu.

“Siku ya Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi alifika kijijini akiwa na askari watatu kwenye gari la Polisi (Difenda) wa Kituo cha Mugumu na kudai kuwa nipo chini ya ulinzi kisha kunifunga pingu, akidai kuwa nilimwibia Deki ya Video na kutoroka nyumbani kwake, walinipandisha kwenye Difenda kunipeleka kituoni “ alisema.

Kijana huyo alieleza kuwa baada ya kufikishwa kituoni Mugumu askari huyo na wenzake walianza kumuhoji huku wakimpa maneno ya vitisho, kijana huyo alipokataa kuwa hakuiba wala kutoroka, Sajenti Fatuma aliamuru kijana huyo kuvulishwa shati alilovaa na kisha akafungwa usoni na kuombwa anyooshe mkono mezani ili apewe 'Sapraizi'.
Ni kidole gumba tu kilicho nusurika kukatwa huku vingine vinne vikifyekwa na panga mkono wa kulia wa Steven Magessa.

"Sekunde chache nilihisi kitu kikali kimenipitia kwenye vidole vyangu vinne vya mkono wa kulia na kufuatiwa na maumivu makali, niliusogeza mkono wangu mdomoni kuupoza kwa kuupuliza ndipo nilipo gundua kuwa nimekatwa kabisa vidole vyangu vinne vya mkono wangu wa kulia ikibakia  dole gumba tu" kijana Steven alisimulia kwa uchungu.
“Niliangua kilio kutokana na maumizu na sijui vidole vyangu hadi sasa sijui vikowapi, askari wenzake baada ya kuona nimetokwa na damu nyingi walimshauri anipeleke hospitali ya Wilaya ya Mugumu ili nipatiwe matibabu kabla ya kuondoka kuja Mwanza,”alisisitiza.

Steven alisema baada ya kupatiwa matibabu, tulienda kupanda basi ili kuja Mwanza kwa madai kuwa amenifungulia kesi ya wizi wa Deki ya Video na tuliopfika alinipeleka kituo cha Polisi Kati Nyamagana na kuniweka Mahabusu akinituhumu wizi, lakini nilipochukuliwa maelezo nilikana tuhuma za wizi na kueleza ukweli wangu ili kupata msaada.

Huku taarifa zingine kutoka ndani ya jeshi zilizopatikana zilidai kuwa askari huyo alikusudia kufanya ukatili huo kutokana na udanganyifu ambao alifanya kwa uongozi wake akiomba kupatiwa silaha (SMG) kwa ajili ya kuitumia kwenye kazi za nje lakini lengo ikiwa ni kwenda na silaha hiyo kwa ajili ya kumkamata na kumtishia kijana huyo, jambo ambalo uongozi ulimgomea.

JESHI LA POLISI LINASEMAJE
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Valentino Mlowola, jana ofisini kwake amethibitisha kuwepo kwa taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa tayari Jeshi hilo limechukuwa hatua madhubuti hatua ya awali ikiwa ni kumshikilia askari huyo kwa kufanya ukatili huo kwa kuvunja sheria na kujichukulia sheria mkononi kumjeruhi kijana huyo.

Mlowola alisema pamoja na kijana huyo awali kufunguliwa jarada la kutuhumiwa kufanya kosa la wizi (Jinai) na kudaiwa kutorokea kijijini kwao, bado askari huyo alitakiwa kufuata mfumo wa kiutawala na kisheria uliopo kushughulikia suala hilo badala ya kuamua kujichukulia maamuzi ya kumwadhibu mtuhumiwa kabla ya uthibitisho wa mashitaka yaliyokuwa yamefungulia.

“Nilipopokea taarifa hizi kwa mashangao na masikitiko makubwa na zimenisitua sana, si kitendo cha kiungwana hata kidogo kwa mtu ambaye anatakiwa kufuata taratibu za mfumo wa utawala na sheria katika utekelezaji wa kushughulikia kero na matatizo ya jamii, alitakiwa kutumia busara kwani tayari aliishamfungulia jarada la kumtuhumu kumwibia ikizingatiwa naye ni mzazi wa watoto watano ni lazima anaujua uchungu,”alisema. 
  
Kamanda Mlowola alieleza kufatia ukatili huo kufanywa na askari wake ameunda timu ya kikosi cha askari kwenda hadi kijijini Magange wilayani Serengeti mkoani Mara ili kufanya uchunguzi wa tukio hili ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na familia, wananchi wa kijiji hicho kisha Hospitali ya Wilaya ya Serengeti alipopatiwa matibabu ya awali.

“Ili tupate ukweli wa jambo hili tumeunda timu hiyo, kwani kijana Steven tumemhoji ametueleza jinsi askari Fatuma alichomfanyia na kudai hakumwibia, lakini askri wetu pia amehojiwa awali amedai hakufanya kitendo hicho bali wananchi ndo walimfanyia ukatili huo hivyo ni mkanganyiko lakini ukweli utapatikana tu japo kuwa tukio hili halikufanyika Mwanza”alisisitiza.

Mlowola alisema kwamba tayari tunamshikiria askari huyu na kumfungulia jarada la uchunguzi kwa taratibu za kijeshi na ikibainika kutenda kosa hilo tutumfukuza kazi na kumfikisha katika vyombo vya sheria ili kuchukuliwa hatua zaidi kulingana na kosa alilofanya, lakini pia kijana Steven naye anashikiriwa kwa tuhuma alizonazo za wizi kufatia jarada lililopo.

“Hatuwezi kuendelea kucheka na kufumbia macho kitendo hiki ni jambo ambalo linamgusa kila mtu hata mimi ni mzazi ukiachana na utumishi wangu wa umma, ntahakikisha jambo hili nalishughulikia kwa umakini na kutoa taarifa kwa umma ili pia kueleza wananchi kuwa tukio hili limefanywa na mtumishi kama mtu si Taasisi ya Jeshi la Polisi na ahidi kutenda haki kwenye hili,”alisisitiza. 

Wito wangu kwa wananchi ni kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuwaadhibu watuhumiwa mbalimbali kabla ya kuthibitika kwa makosa na tuhuma hizo, lakini wazingatie kufuata taratibu za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili kushughulikia matatizo yao nawaomba waendelee kutoa ushirikiana na kufuata mfumo uliopo badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.