ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, April 26, 2026

YANGA WATINGA FAINALI, MACHO SASA KWA DABI NZITO INAYOFUATA?

 


Mabingwa watetezi, Young Africans SC wamefanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Muungano 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa usiku wa Jumamosi, Aprili 25, 2026 kwenye dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.

Yanga walionyesha dhamira mapema baada ya mshambuliaji wao raia wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 9 akiitungua timu yake ya zamani. Kiungo mahiri raia wa DR Congo, Maxi Mpia Nzengeli akaongeza bao la pili dakika ya 25, akiipa Yanga utulivu wa mchezo.

Kwa upande wa Azam FC, kiungo mshambuliaji Feisal Salum Abdallah alifunga bao la kufutia machozi dakika ya 78, naye akiiumiza klabu yake ya zamani, lakini halikutosha kuizuia Yanga kusonga mbele.

Sasa Yanga wanasubiri kumjua mpinzani wao wa fainali atakayepatikana katika mchezo wa nusu fainali ya pili kati ya Simba SC na Mlandege FC utakaopigwa leo kuanzia saa 2:15 usiku, uwanja huo huo wa Amaan.

Fainali ya Kombe la Muungano 2026 imepangwa kupigwa Jumatano, Aprili 29, saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan .

Hata hivyo, macho ya mashabiki wengi tayari yanaelekezwa mbele zaidi kwani siku tatu tu baada ya fainali hiyo, kunatarajiwa kuchezwa dabi kubwa ya watani wa jadi, Simba SC dhidi ya Young Africans SC mchezo unaotarajiwa kuwa na presha, ushindani mkali, na huenda ukaathiriwa moja kwa moja na matokeo ya fainali ya Muungano.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment