ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, March 6, 2026

WANAWAKE WATAKIWA KUVAA UJASIRI WA KUPIMA AFYA ZAO.

 Wanawake watakiwa kuvaa ujasiri wa kupima afya zao


Hofu ya kupima afya imetajwa kuwa kitanzi kwa wanawake wengi, kwa kuwa imesababisha baadhi kuteseka hata kupoteza maisha kwa magonjwa makubwa ikiwamo kansa, ambayo yakigundulika mapema wangepata tiba.

Imeelezwa kuwa wengi hulazimika kupima wakiwa tayari kwenye hali mbaya, ikiambatana na maumivu.
 
 Hivyo wanawake wametakiwa kubadili mtazamo, na kujenga tabia ya kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya mapema.

Akizungumza katika kongamano la afya ya wanawake lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mkemia na Mtafiti wa Miti Dawa, Prof. Faith Mabiki, alisema bado kuna hofu kubwa miongoni mwa wanawake kuhusu vipimo vya afya licha ya maendeleo ya teknolojia katika sekta ya tiba.

Prof.Mabiki alisema magonjwa kama saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti yanaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa, endapo yatagunduliwa mapema kupitia vipimo vya mara kwa mara.

“Wanawake wengi huweka afya zao kama jambo la pili, lakini ukweli ni kwamba afya njema ndiyo msingi wa ustawi wa familia na maendeleo ya jamii,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA, Faraja Kamendu, alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na menejimenti ya chuo kuhakikisha wafanyakazi wanawake wanapata elimu ya afya na huduma muhimu za kitabibu.

Kamendu alisema semina hiyo imewapa wanawake fursa ya kujifunza kuhusu changamoto mbalimbali za kiafya pamoja na njia za kujikinga nazo.

Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya SUA, Dk.Graca Chotamawe, alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka duniani, ikiwamo barani Afrika kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Alisema takribani watu milioni 41 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa hayo, huku sababu zake zikitajwa kuwa ni pamoja na kupungua kwa mazoezi, matumizi ya vyombo vya usafiri kama magari na bodaboda, pamoja na matumizi ya dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa magonjwa hayo huongeza mzigo wa kiuchumi kwa familia nyingi, kwa kuwa matibabu yake huchukua muda mrefu na kugharimu fedha nyingi.

Kongamano hilo lilihusisha watumishi wanawake wa SUA na wanafunzi, huku pia likitoa fursa ya upimaji wa afya kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo presha na sukari.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment