![]() |
| Daraja la Ubagwe laondoa adha ya mafuriko Ushetu |
Wananchi wa Wilaya ya Ushetu sasa wana sababu ya kutabasamu baada ya kukamilika kwa Daraja la Ubagwe, mradi muhimu wa miundombinu uliokuja kuondoa changamoto ya muda mrefu ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa msimu wa mvua.
Kwa miaka mingi wakazi wa eneo hilo walikuwa wakikumbwa na adha kubwa hasa kipindi cha mvua kali. Mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El-Nino yaliwahi kuharibu miundombinu ya barabara na kukata kabisa mawasiliano kati ya maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo pamoja na mikoa jirani ya Tabora, Geita na Shinyanga. Hali hiyo ilifanya shughuli za kiuchumi kudorora huku wananchi wakipata hasara kubwa.
Wakulima walishindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, wafugaji walikwama kuvusha mifugo yao na wafanyabiashara walipoteza fursa za kibiashara kutokana na kukosekana kwa njia salama ya kuvuka. Changamoto hiyo pia iliathiri huduma za kijamii, ambapo baadhi ya wagonjwa walishindwa kufikishwa hospitalini kwa wakati.
Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo, hali hiyo ilikuwa hatari zaidi kwa akina mama wajawazito ambao wakati mwingine walilazimika kuvuka katika mazingira magumu au kushindwa kabisa kuvuka, jambo lililosababisha vifo katika baadhi ya matukio.
Hata hivyo, matumaini mapya yameanza kuonekana baada ya kukamilika kwa Daraja la Ubagwe, mradi uliogharimu shilingi bilioni 13.5. Daraja hilo linatajwa kuwa mkombozi wa wananchi wa Ushetu na maeneo ya jirani kwa kuwa sasa linahakikisha mawasiliano yanakuwepo wakati wote wa mwaka bila kujali msimu wa mvua.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua daraja hilo, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, amesema kukamilika kwa daraja hilo kumesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikiwakumba wananchi kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Kihongosi amebainisha kuwa ujenzi wa Daraja la Ubagwe umefanyika sambamba na ujenzi wa madaraja mengine mawili ya Kasenga na Ng’hwande, hatua inayolenga kuboresha zaidi mtandao wa usafiri na mawasiliano katika ukanda huo.
Amesema kwa sasa daraja hilo lipo katika kipindi cha majaribio ili kuhakikisha linakidhi viwango vya ubora na thamani ya fedha iliyotumika kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa matumizi ya wananchi.
Akizungumzia ubora wa mradi huo, Kihongosi amesema thamani ya fedha inaonekana wazi kupitia ubora wa ujenzi wake, huku akiwataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Katika ziara hiyo pia amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa maendeleo ya miundombinu na ustawi wa shughuli za kiuchumi kama kilimo, ufugaji na biashara hutegemea uwepo wa amani.
Kwa kukamilika kwa Daraja la Ubagwe, wananchi wa Ushetu wanatarajia kuona ongezeko la shughuli za kiuchumi, urahisi wa usafiri na mawasiliano pamoja na kuboreshwa kwa upatikanaji wa huduma za kijamii, jambo litakalosaidia kuharakisha maendeleo ya eneo hilo na ukanda wa Ziwa kwa ujumla.
Ujenzi wa daraja hilo ni mfano wa namna uwekezaji katika miundombinu unavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi kwa kuondoa vikwazo vya kijiografia na kuleta fursa mpya za maendeleo.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment