NA VICTOR MASANGU/PWANI
HABARI IMESOMWA NA ALBERT G.SENGOMAKAMU mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dogo Mabrouk ameongoza mbio za Samia Marathon iliyofanyika Ijumaa ya Februari 22,2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani Mlandizi Kibaha Vijijini.
Mabrouk ameongoza mbio hizo akimwakilisha Waziri mkuu Kassim Majaliwa ambaye ndiye alipaswa kuwa mgeni rasmi katika kuongoza mbio hizo.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Dogo Mabrouk akizungumza na washiriki wa mbio za Samia Marathon .
Mabrouk katika mbio hizo ameongozana na viongozi wa chama na Serikali akiwemo mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa Hamoud Jumaa ( MNEC) ambaye ni mkazi wa mji wa Mlandizi, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Mwishehe Mlao, mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na katibu tawala mKoa wa Pwani Rashid Mchatta.
Akiwa katika mbio hizo Mabrouk alikimbia umbali wa kilomita tano ikiwa ni kutoka uwanjani hapo kupitia barabara ya ofisi ya CCM Mlandizi, kituo cha Afya Mlandizi na kurudi uwanja ambapo akiwa uwanjani hapo alishuhudia mashindano mbalimbali yakiwemo ya kukuna nazi.
Akizungumza na wananchi walioshiriki mbio hizo , Mabrouk amesema kuwa lengo la mbio za Samia Marathon ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajia kufanyika mwishoni mwaka mwaka huu.
Washiriki wa Samia Marathon wakifanya mazoezi mbalimbali katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani Mlandizi
Mabrouk amesema ameona watu wengi wamejitokeza katika kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura lakini mara nyingi kujitokeza kupiga kura wanakuwa wazito ndio maana watatumia mbio hizo kutoa elimu na kuhamasisha Wananchi kupiga kura.
"Nawaomba watu wote waliokuja hapa katika mbio hizo tujitahidi kuhakikisha tunajitokeza pia siku ya kupiga kura katika kuwachagua viongozi wetu akiwemo Rais, Wabunge na Madiwani,"amesema Mabrouk.
Katika hatua nyingine Mabrouk amesema kuwa serikali ya awamu ya sita inaongozwa na mwanamke ambaye ni Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo makubwa hivyo amewaomba wananchi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Hamoud Jumaa, (MNEC) amesema kuwa mbio za Samia Marathon ni utekelezaji na makubaliano maalum ya viongozi wake wa juu katika kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kujitokeza katika kupiga kura ya kuwachagua viongozi wao.
Baadhi ya Viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) , wananchi katika mazoezi ya mbio za Samia Marathon.
Jumaa amesema kuwa kufanyika kwa mbio za Samia Marathon katika mji wa Mlandizi ni sehemu ya majaribio lakini wanategemea kufanya maandalizi ya mbio hizo kwa miaka mingine ya mbele katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Pwani.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mKoa wa Pwani Josian Kituka, ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha kufanyika kwa Samia Marathon huku akiomba na wengine wajitokeze zaidi katika kuendeleza mbio hizo.
Hatahivyo, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge , ametumia nafasi ya mbio za Samia Marathon kueleza mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wake huku akisema suala la umeme Vijijini imefikia asilimia 98 huku maji yakifikia asilimia 83 na asilimia zilizobaki zitakamilika mwaka huu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.