ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 13, 2023

SADC: MAKATIBU WAKUU WA SADC WAKUTANA KINSHASA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC ngazi ya Makatibu Wakuu akiwa katika meza ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa SADC unaofanyika Kinshasa, Jamhui ya Kidemokrasia ya Congo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu, Balozi Songhu Kayumba akisoma hotuba ya ufunguzi ya kikao hicho.
 Wajumbe wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanaoshiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa SADC, ngazi ya Makatibu Wakuu unaofanyika Kinshasa, Jamhui ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) umefunguliwa leo tarehe 13 March 2023 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina  Shaaban.

Wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC, Balozi Songhu Kayumba alisisitiza umuhimu wa wajumbe kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yatakayolenga kufanikisha utekelezaji wa agenda  zitakazojadiliwa.

Makatibu Wakuu wanajadili agenda mbalimbali ambazo ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali waliyotoa katika Mikutano iliyopita.

Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye Mkutano huo na imejipanga kusukuma utekelezaji wa agenda ilizoziibua au kuziunga mkono katika mikutano iliyopita.

 Agenda hizo ni pamoja na: ujenzi wa sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambalo litasimikwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU); Tafsiri ya Nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili ambayo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye Jumuiya; Mpango wa Kanda wa Ununuzi wa Pamoja wa Bidhaa za Afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD); na Mkakati wa pamoja wa Kanda wa Kusimamia Sekta ya Mbolea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri  utakaofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 Machi 2023 baada ya Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilika.


Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.