Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus
Mwamanga (picha ya juu na chini )
akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake
nchini Bi. Bella Bird katika hafla ya kuagana naye .
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus
Mwamanga (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuagana na
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia aliyemaliza muda wake, Bi. Bella Bird
alipofika kwenye ofisi ndogo za Mfuko huo jijini Dar es Salaam kuagana na
wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa TASAF
wakimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird (hayupo pichani
) wakati alipofika katika taasisi hiyo kuagana nao baada ya kumaliza muda wake
nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bw.Ladislaus
Mwamanga (aliyevaa tai) akimwongoza Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia
anayemaliza muda wake bi. Bella Bird kuingia katika ukumbi wa mikutano wa TASAF
katika ofisi ndogo jijini Dar es Salaam.
Na Estom Sanga- TASAF- DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake Bi.Bella Bird amepongeza jitihada za serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF- kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kukabiliana na umaskini nchini.
Bi.Bella Bird amesema Tanzania imepata mafanikio makubwa
katika azma ya kuwaondolea wananchi wake kero ya umaskini jambo ambalo
amesema limeijengea heshima kubwa serikali na hivyo kufanya mataifa
mengine hususani ya bara la Afrika kuwavutiwa nayo.
Mkurugenzi
Mkazi huyo wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake ameyasema hayo
alipokutana na Wafanyakazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- katika
Ofisi ndogo ya Mfuko huo jijini Dar es salaam ambako alikwenda kuagana
nao baada ya kumaliza kipindi chake cha takribani CHA utumishi wa miaka
minne hapa nchini.
‘’ mataifa mengine ya Afrika yamekuwa yakija
Tanzania kujifunza namna TASAF ilivyofanikiwa kuwafikia watu maskini
kabisa kupitia Mpango wake wa Kunusuru Kaya Maskini’’ amesisitiza Bi.
Bella Bird.
Amesema tafiti huru za ndani na nje ya nchini
zilizofanywa zinaonyesha kuwa umaskini nchini Tanzania umepungua katika
kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuwa
kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kuwa mafanikio hayo yanalindwa,
kuboreshwa na kuendelezwa.
Bi.Bella Bird amesisitiza kuwa Benki
ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na
kuongeza kuwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali
kupitia TASAF ni miongoni mwa miradi hiyo.
Akizungumza katika
hafla hiyo fupi Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga
ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira yaliyosaidia Benki
ya Dunia kukubali kufadhili shughuli za Mpango was Kunusuru Kaya
Maskini.
Bwana Mwamanga amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya
sehemu ya kwanza yamewezesha Serikali kukubali kutekeleza sehemu ya pili
ambayo inatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli baadaye mwezi ujao.
Mkurugenzi
Mtendaji huyo wa TASAF ameahidi kuwa taasisi hiyo imejipanga vizuri
kuhakikisha kuwa sehemu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali
huku Mkazo ukiwekwa katika kuwashirikisha Walengwa katika kutekeleza
miradi ya Maendeleo kwenye maeneo yao na kisha kulipwa ujira kama sehemu
ya kuwaongezea kipato .
Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF ulianzishwa na
Serikali kwa lengo la kusaidia wananchi kupitia utaratibu wa Kaya
Maskini sana ili ziweze kujikimu kwa kupata mahitaji muhimu yakiwemo
lishe, elimu na afya huku mkazo ukiwekwa katika kuziwezesha kaya za
Walengwa kutumia sehemu ya ruzuku kuanzisha miradi midogo midogo ya
uzalishaji mali ili kuinua kipato chao na kuboresha maisha yao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.