Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mashambulio ya makombora yaliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika kambi mbili za Marekani nchini Iraq ni kibao cha uso tu alichopigwa adui huyo.
Amesema, majibu ya Iran hayatoishia hapo kwani kinachotakiwa hasa ni kuangamizwa kikamilifu uwepo wa kifisadi na kiharibifu wa Marekani katika eneo hili zima.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo asubuhi (Jumatano) wakati alipoonana na maelfu ya wananchi wa Qum na huku akitilia mkazo uhakika kwamba mataifa ya eneo hili na tawala zilizotokana na wananchi, bila ya shaka yoyote hazitaki kuona Marekani inaendelea kuwepo katika eneo lao, amesema, kuwepo Wamarekani kwenye eneo hili na katika sehemu yoyote ile duniani hakuna matokeo mengine isipokuwa vita, ugomvi, fitna na kuharibiwa miundombinu ya eneo hilo.
Vile vile amezungumzia nafasi ya kipekee isiyo na mbadala ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika kufelisha njama za Marekani huko Palestina, Iraq na Lebanon na kuongeza kuwa, shahid Luteni Jenerali Soleimani alifanikiwa kuvunja na kufelisha njama zote za Marekani zilizotumia fedha nyingi, mabavu, uchochezi wa kisiasa na uundaji wa makundi mbalimbali.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, tunaposema "adui" tunakusudia Marekani, utawala wa Kizayuni na majimui ya vibaraka wao na kuongeza kuwa, baadhi ya tawala za ndani na nje ya eneo hili hazipaswi kuingizwa kwenye kundi hilo la adui hadi pale zitakapochukua hatua ya kumtumikia adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kuwa, muswada uliopasishwa na bunge la Iraq wa kufukuzwa wanajeshi wa Marekani nchini humo ni hatua nzuri sana na tunamuomba Mwenyezi Mungu alete taufiki ya kuendelea jambo hilo katika nchi nyinginezo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.