Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, watu 6,000 walipoteza maisha kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa surua (measles) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwaka uliomalizika 2019.
WHO imetoa mwito wa kupatiwa fedha zaidi ili kupambana na mlipuko huo unaoaminika kuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kufikia sasa, WHO imeweza kupokea dola milioni 27.6 za Marekani, ingawaje inahitaji dola milioni 40 zaidi ili kupanua shughuli ya kutoa chanjo kwa watoto kati ya miaka 6 na 14, katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Dakta Amedee Prosper Djiguimde, afisa wa Shirika la Afya Duniani nchini Kongo DR amesema, "Maelfu ya familia za Wakongomani wanahitaji misaada yetu ili kuzikwamua kutoka kwenye mgogoro huo wa kiafya. Hatuwezi kufanya chochote iwapo hatuna fedha."
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), asilimia 74 ya wagonjwa hao wa surua ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na mbaya zaidi ni kuwa, takribani asilimia 90 ya vifo ni watoto wa umri huo.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka uliomalizika wa 2019, takribani maambukizi laki 3 yanayodhaniwa kuwa ni ya surua yaliripotiwa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.