Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) imewataka watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutodanganyika na kuacha kutumia dawa kupunguza makali ya VVU kwani hakuna mbadala wa ARV.
Rai hiyo imetolewa leo Juni 28,2019 na Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango wakati akifunga Kambi ya Ariel 2019 iliyoandaliwa na asasi inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI).
Akizungumza kwenye kambi hiyo iliyojumuisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Mara Bw. Issango alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa watu wengine wanaacha kutumia ARV na kisha kujikita kwenye dawa za kienyeji au maombi. “Matokeo yake ni VVU kuendelea kuwashambulia. Kinachosaidia kupunguza makali ya VVU mwilini ni ARV peke yake, hakuna mbadala,” alisisitiza.
Mkurugenzi huyo alisema, “Msidanganyike mkaacha kutumia dawa za ARV, mpaka sasa bado wanasayansi hawajapata dawa nyingine. Tunaamini ipo siku dawa itapatikana lakini kwa sasa wenye maambukizi ya VVU endeleeni kuwa wafuasi wazuri wa dawa na mtumie kwa usahihi.”
Akizungumzia vita dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kazi ambayo asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) imekuwa ikiifanya tangu kuanzishwa kwake, Mkurugenzi huyo alisema kuwa hicho ni kipaumbele cha taifa hivyo hakina budi kufanyiwa kazi kwa juhudi.
Alisema kwa watoto na vijana wenye maambukizi, wataendelea kupata huduma za matunzo na tiba bila ubaguzi wowote ili kuhakikisha kuwa afya zao zinaendelea vizuri hivyo kuweza kufikia ndoto zao za baadaye.
“Kwa kazi zenu, AGPAHI mnagusa maisha ya Watanzania wengi. Kitendo cha kusaidia upatikanaji wa huduma za matunzo na tiba kwa wanaoishi na VVU ni cha utu. AGPAHI ni asasi ya kiutu na inajali Watanzania. Tunawashukuru kwa kuendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma hizi muhimu,” alisema.
Aidha alikumbusha kwamba kuwa na maambukizi ya VVU siyo changamoto ya kumzuia mtu anayeishi na VVU kusonga mbele katika maisha yake na kutimiza ndoto zake, “Kinachotakiwa ni kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya,” alisema.
Kutokana na umuhimu wake, Bw. Issango aliziomba serikali za mikoa ambako AGPAHI inafanya kazi kushirikiana na asasi hiyo kikamilifu ili kuendelea kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU.
Wakisoma risala yao, washiriki wa Ariel Camp 2019 waliiomba serikali kuiunga mkono AGPAHI ili huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana ziendelezwe na kuenezwa nchi nzima hivyo kuwafikia watoto wengi zaidi.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango akifunga Kambi ya Ariel 2019 iliyoandaliwa na asasi inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) leo katika ukumbi wa Landmark Hotel jijini Dar es salaam. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Meneja Mawasiliano wa AGPAHI, Bi. Agnes Kabigi akizungumza wakati wa kufunga Ariel Camp 2019 iliyoanza Juni 23,2019.
Keki maalumu kwa ajili ya washiriki wa Kambi ya Ariel 2019.
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango na watoto wakikata keki ya Kambi ya Ariel 2019.
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango akilishana keki na mtoto aliyeshiriki Kambi ya Ariel 2019.
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango akiendelea na zoezi la kuwalisha keki washiriki wa Kambi ya Ariel 2019.
Kijana wa sarakasi kutoka kundi la Baba Watoto akitoa burudani ya kuzungusha meza kwa kutumia miguu wakati wa kufunga Kambi ya Ariel 2019.
Mshiriki wa Ariel Camp 2019 akitoa burudani ya kuimba.
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango akimkabidhi mtoto zawadi ya begi lenye vifaa vya shule.
Zoezi la kugawa zawadi likiendelea.
Vijana wakiangalia zawadi ya mabegi waliyopewa.
Walezi watoto nao walipata zawadi.
Mkurugenzi wa Uraghbishi na Habari wa TACAIDS, Bw. Jumanne Issango akiangalia michoro mbalimbali iliyochorwa na washiriki wa kambi ya Ariel 2019 inayoelezea historia ya maisha yao na ndoto zao katika maisha.
Washiriki wa Kambi ya Ariel 2019 wakiwa katika picha ya pamoja.
Washiriki wa Kambi ya Ariel 2019 wakiwa katika picha ya pamoja wakionesha zawadi ya mabegi yao.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.