ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, November 5, 2018

VIDEO:- AGPAHI YATOA MSAADA WA MAGARI KUBORESHA HUDUMA UDHIBITI VVU NA UKIMWI MWANZA


Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa John Mongella, akikata utepe wakati wa hafla ya makabidhiano ya magari yaliyotolewa na AGPAHI kwa ajili ya kuboresha huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri ya wilaya ya Buchosa na Misungwi mkoani Mwanza.



GSENGOtV
Asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Initiative (AGPAHI) inayolenga kutokomeza UKIMWI kwa watoto na familia nchini Tanzania imetoa msaada wa magari mawili aina ya Nissan Patrol kwa halmashauri za wilaya za Buchosa na Misungwi mkoani Mwanza kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri hizo.

Magari hayo yenye namba za usajili DFPA 7015 na DFPA 7016 yana thamani ya shilingi milioni 186 yamenunuliwa na shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) chini ya vituo vya Kudhibiti Magonjwa na Kinga (CDC).

Hafla fupi ya Makabidhiano ya magari, imefanyika leo Jumatatu Novemba 5,2018 wakati wa kikao cha wadau wa afya na ustawi wa jamii mkoa wa Mwanza kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa John Mongella.

Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo kwa Mkuu huyo wa mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI, Dkt. Sekela Mwakyusa alisema msaada huo wa magari ni kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma za afya hususani za VVU na UKIMWI kwenye vituo vya kutolea huduma.

Dkt. Mwakyusa alisema, AGPAHI imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na halmashauri katika kuboresha huduma za VVU na UKIMWI kwa ajili ya ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Magari tuliyokabidhi leo yana thamani ya shilingi milioni 186, na hii ni sehemu ya vyombo vya usafiri (magari,pikipiki na baiskeli) vyenye thamani ya shilingi milioni 900.2 tulivyonunua katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2017 hadi Septemba 2018 kwa ajili ya kuleta tija kwenye utendaji kazi ili kuboresha huduma za VVU na UKIMWI katika halmashauri ambazo AGPAHI inafanya kazi,” alieleza Dkt. Mwakyusa.

Aliongeza kuwa katika jitihada za kuboresha utoaji wa huduma za VVU na UKIMWI, katika kipindi hicho, AGPAHI imefanyia ukarabati vituo 146 vya kutolea huduma vikiwemo 36 vya mkoa wa Mwanza. Pia imeweka mifumo ya umeme jua kwenye vituo 40 vya kutolea huduma kwenye halmashauri mbalimbali.

Akipokea magari hayo, Mkuu wa mkoa, Mheshimiwa Mongella aliishukuru AGPAHI kwa kuwa mdau muhimu katika sekta ya afya na kuomba waendelee kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Mongella aliwataka watendaji wa halmashauri zilizopewa magari kutunza na kuyatumia magari hayo kwa kazi za afya na maendeleo ya halmashauri na siyo vinginevyo.


Muonekano wa nyuma magari yaliyotolewa na AGPAHI.
 Mkurugenzi wa AMREF Tanzania Florence Temu akiwasilisha jinsi shirika lake lilivyo shiriki katika utoaji huduma za Afya na Kupambana na VVU, kuelekea Disemba mosi 2018.
Shukuran.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.