ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 21, 2018

HATIMAYE ABDUL NONDO AMEFIKISHWA MAHAKAMANI MKOANI IRINGA

Hatimaye Abdul Nondo amefikishwa Mahakamani Iringa Tanzania
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo amesafirishwa usiku wa kuamkia leo Machi 21, 2018 kupelekwa mkoani Iringa.
Taarifa zilizotolewa na wakili wake, Jebra Kambole leo Jumatano zinaeleza kuwa sasa Nondo yupo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa.
Nondo anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha Machi 6, 2018 na siku inayofuata akaonekana mjini Mafinga, wilayani Mufindi, Iringa ambako alishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo na baadaye kurejeshwa Dar es Salaam.
Tangu akamatwe Nondo hajawahi kuzungumza na wakili wake wala mtu yeyote wa karibu yake jambo ambalo limekuwa likipingwa na watetezi wa haki za binadamu.
Jana, Jebra alisema kuwa wamefungua kesi ya kuiomba mahakama kumpa dhamana Nondo, kutoa amri ya kuwapa mawakili haki ya kuonana naye na kuitaka mahakama itamke mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ameshtakiwa kinyume cha sheria.
Kumekuwepo kesi kadhaa za kutoweka watu hususan wanasiasa nchini Tanzania suala ambalo limezusha wasiwasi kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama nchini humo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.