Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kutoka kushoto) akikagua moja ya shimo la dhahabu kwenye machimbo ya Buhemba.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi wakati wa ziara yake kwenye eneo la machimbo ya dhahabu la Buhemba, Wilayani Butiama, Mkoani Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) kuzungumza na Wachimbaji (hawapo pichani). Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini (FEMATA), John Bina.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba.
Baadhi ya Wachimbaji kwenye Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani).
UKAGUZI
MACHIMBO YA BUHEMBA KUKAMILIKA KABLA JANUARI 10, 2018
Serikali imeagiza
kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu
ya Buhemba, Wilayani Butiama Mkoani Mara uwe umekamilika ili shughuli za
uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo alitoa agizo hilo Desemba 27, 2017 alipofanya ziara
kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na
kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao hadi hapo
ukaguzi utakapokamilika.
“Ninasikitika kuona
shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli
za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema.
Serikali ilisitisha
shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya
kutokea vifo vya wachimbaji Watatu na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na
kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.
Nyongo alisisitiza
kwamba mgodi huo hautofunguliwa hadi hapo zoezi la ukaguzi litakapokamilika.
“Hatuwezi kuufungua mgodi huu leo hii bila kukamilisha zoezi la ukaguzi kwahiyo
kabla ya Tarehe 10 mwezi ujao, Wakaguzi wawe wamekamilisha ili mgodi uanze kazi
na shughuli za uchumi zilizokuwa zikifanyika mgodini hapa zirejee,” alisema.
Alisema shughuli hiyo
ya Ukaguzi inapaswa kukamilika mapema ili maduara yasiyo salama yaweze
kutambulika na yazuiwe na yaliyokuwa salama yafahamike na kuendelezwa.
Nyongo alikumbushia agizo alilotoa kwa
Wakaguzi wa Migodi Desemba 14, 2017 Mkoani Tabora
alipotembelea kwenye Mgodi wa Dhahabu wa Nsungwa Gold Mine uliopo katika Kata
ya Silambo Wilaya ya Kaliua la kukagua hali ya usalama na kuwasaidia Wachimbaji
kuepusha ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.
“Ninawaagiza kwa mara nyingine
Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili
kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.
AIDHA, kwa
upande mwingine, Naibu Waziri Nyongo amewataka Wachimbaji wa Madini kote nchini
kutambua
wajibu wao wa kulipa Tozo na Kodi mbalimbali Serikalini kwa ajili ya maendeleo
yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema Serikali
haina kikwazo na wachimbaji wadogo na inafanya jitihada za kuwasaidia kuwa na
uchimbaji wenye tija hata hivyo alisema wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulipa
kodi ambayo itawanufaisha wao kama wachimbaji lakini pia Jamii inayozunguka
maeneo yenye migodi na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa
Rasilimali Madini ni kwa ajili ya Watanzania wote na kwamba kila Mwananchi
anayo haki ya kunufaika nayo kwa namna moja ama nyingine mojawapo ikiwa ni
manufaa yatokanayo na kodi zinazolipwa kutokana na shughuli za uchimbaji.
“Serikali inahitaji ipate
kodi yake kwani madini yanapaswa kuwaneemesha Watanzania wote. Mtakavyolipa
kodi, fedha husika zitatumika kuwaletea na kuwaboreshea huduma mbalimbali
ikiwemo elimu, afya na miundombinu mbalimbali,” alibainisha Naibu Waziri
Nyongo.
Aliongeza kuwa lengo
la Serikali ni kuwarasimisha Wachimbaji
wa Madini kwa kuwapatia Leseni za Uchimbaji ili wachimbe kwa kufuata utaratibu
unaotakiwa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho
yake ya Mwaka 2017.
Naibu Waziri Nyongo
yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku mbili ya kukagua shughuli za uchimbaji wa
madini kwenye maeneo mbalimbali yenye migodi pamoja na kuzungumza na wachimbaji
ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.