Waziri MkuuKassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja
na maofisa wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za
umma
Waziri Mkuu amewasimamisha kazi maofisa hao leo Julai 23, 2017 wakati
alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye
ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi na
pia amemtaka Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) mkoa wa Songwe, Bw. Damian Sutta kuwakamata na kuanza
kuwachunguza haraka maofisa hao na kisha ampelekee taarifa ofisini
kwake.
Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa
Halmashauri hiyo Bw. Simon Noel, Bw. Bahati Chomoka ambaye ni Cashier
na Bw. Remmy Haule ambaye ni Ofisa Ugavi.
Waziri Mkuu amesema Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya
magari ya Serikali kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo
hazikusajiliwa na wala hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo
halikubaliki.
Amesema Kampuni ya Umbwila ni moja kati ya Kampuni zinazolipwa fedha
nyingi za utengenezaji wa magari ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi huku
ikiwa haina sifa za kufanya kazi hiyo ya utengenezaji magari.Kampuni
zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni Garage.
"Mfano duka la Umbwila ambalo linauza vipuri vya magari lakini
Halmashauri inalilipa fedha kwa ajili ya utengenezaji wa magari jambo
ambalo si sahihi kwa sababu lile ni duka la vipuri na si gereji.
Wanamlipa muuza vipuri kama mtengeneza magari"
Waziri Mkuu ameongeza kuwa "hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo
haikubaliki kwani watu tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo
vya rushwa na ufisadi. Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi."
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,
Mheshimiwa Eric Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani
ya Halmashauri hiyo na kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye
uaminifu na nidhamu.
"Halmashauri inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona
Halmashauri hii na zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali
hii no, hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi. Serikali haiwezi
kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana wakijinufaisha kwa fedha za
umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma
mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu".
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.