ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 14, 2017

KANDA YA ZIWA KUNEEMEKA NA MIKOPO YA TADB

 Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella (kulia) akizungumza na viongozi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) walipomtembelea Ofisini kwake jijini Mwanza. Viongozi hao walikuwa kwenye ziara rasmi ya kukabidhiwa jengo litakalotumiaka kama Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (wapili kushoto).
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella (hayupo pichani) wakati wa ziara rasmi ya kukabidhiwa jengo litakalotumiaka kama Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa.
 Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella (mwenye kofia) akifuatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (aliyevaa) kuelekea kwenye makabidhiano ya jengo litakalotumiaka kama Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa. 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (mbele kulia) akipokea funguo za  kukabidhiwa jengo litakalotumiaka kama Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa  kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Majengo ya Serikali mkoa wa Mwanza, Mhandisi Yohana Mashausi (kushoto). Wanaoshuhudia ni Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella (mwenye kofia) na Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Augustino Matutu Chacha (kulia).

Kanda ya Ziwa kuneemeka na Mikopo ya TADB
Na Mwandishi wetu,
Katika kutimiza ahadi ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria kuwaneemesha wakulima wa Kanda ya Ziwa kwa kufungua Ofisi ya Kwanza ya Kanda yenye lengo la kuwapatia mikopo yenye gharama nafuu wakulima wa Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa makadhiano ya jengo litakalotumika kama Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella alisema kuwa Benki ya Kilimo ikiwa ni taasisi ya umma ina wajibu kusaidia juhudi za Serikali katika kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania hasa katika kuchagiza mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo, ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini na pia kutoa kiasi cha zaidi ya  asilimia 65 cha mali ghafi kwa ajili ya viwanda vya nchi.
“Uanzishwaji wa TADB unatokana na Serikali kutambua umuhimu wa uwekezaji wenye tija kwenye maeneo yote ya sekta ya Kilimo na kuleta mapinduzi ya dhati ya Kilimo ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo na mitaji ya riba nafuu  ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mabenki na taasisi zingine za fedha nchini kutoa mikopo zaidi kwenye sekta ya Kilimo,” amesema.
Mhe. Mongella alisema kuwa Kanda ya Ziwa ina utajiri mkubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ambayo ni mojawapo wa minyororo ya thamani ya mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao mbalimbali na Benki ya Kilimo.
Aliongeza kuwa maendeleo ya sekta ya kilimo inahitaji msaada mkubwa wa uwezeshwaji wa mikopo kutoka TADB kwa kuzingatia kuwa ni chombo cha serikali kilichoanzishwa ili kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania.
“Kwa kutambua jukumu kubwa la TADB katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka   kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini, Ofisi ya Mkoa wa Mwanza iliona kuna umuhimu wa kuipatia Benki hii jengo hili iweze kuwafikia wakulima wa Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani,” aliongeza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Francis Assenga alisema Benki ya Kilimo imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
Bw. Assenga aliongeza kuwa TADB imejipanga kutekeleza malengo ya Serikali katika kuanzisha Benki hiyo ili kusaidia kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika  kilimo nchini.
“Kanda ya Ziwa ni eneo la kimkakati hivyo ujio wetu ni kutimiza dhamira ya dhati ya serikali katika kutatua changamoto za ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo  na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema.
Aliongeza kuwa Benki ya Kilimo imejipanga kushirikiana na Serikali, wabia wa kimkakati na wadau wengine katika kuendeleza sekta ya kilimo, hasa kuboresha na kutekeleza na juhudi zozote sera zinazohusiana na kuhisha ushiriki wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.