Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kushoto akiwakabidhi watendaji wa halmashauri madawati katika hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari miembe saba. |
NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
IMEELEZWA tatizo la kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya mji wa Kibaha lilikuwa linasababishwa na wanafunzi wengine kujisomea wakiwa wamekaa chini ya sakafu sambamba na kuwepo katika mazingira ya miundombinu ambayo sio rafiki kwao hivyo kujikuta wanashindwa kutimiza malengo yao.
Hayo yamebainishwa na wanafunzi wa shule ya sekondari Miembe saba waliohudhuria katika halfa fupi za ugawaji wa madawati ambayo yametolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dr. John Magufuli la wanafunzi wote nchini kuhakikisha wanasoma wakiwa wamekaa kwenye madawati.
Wanafunzi hao akiwemo Ayoub Joseph,Paul Kisige pamoja na Riziki Ismail walisema kwamba kitendo cha baadhi yao kujisomea wakiwa sakafuni kimepelekea kupunguza uwezo wa kifikiri na kujikuta wanafanya vibaya katika masamo yao na kushindwa kufaulu, hivyo wameipongeza serikali ya Rais Dr John Pombe Magufuli kwa juhudi wanazozifanya za kupambana na adha ya madawati.
“Hapo mwanzoni kwa kweli hali ilikuwa ni ngumu sana kwa sababu wanafunzi wengine walikuwa wansoma wakiwa wanakaa chini ya sakafu na hii kiukweli unamwondolea kabisa uwezo wa kufanya vizuri mwanafunzi, lakini kutokana na agizo hili la Rais tumepata nafuu kubwa na wanafunzi tuna imani tutaweza kufanya vizuri katika masomo yetu, na pia tunampongeza mbunge wetu kwa juhudi zake za kutuletea madawati,”walisema wanafunzi hao.
Pia walisema kwamba pamoja na changamoto ya kuwepo kwa upungufu wa madawati lakini serikali inatakiwa kuhakikisha inatilia mkazo suala linguine la nyumba za walimu pamoja na kuimarisha mambo mengine ya msingi, kama kuongeza madarasa mwengine ili kuweza kuepukana na mlundikano kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka katika hotuba yake ya kukabidhi madawati hayo amewataka wanafunzi pamoja na walimu kuachana na tabia ya kuhujumu na kuiharibu miundombinu ya shule na badala yake wahakikishe wanatunza mali zote za serikali kwa lengo la kuweza kuwasaidia watoto wengine wa vizazi vijavyo waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Aidha Koka katika hatua nyingine amebainisha kwamba madawati hayo 537 ambayo ameyatoa katika jimbo lake yataweza kuwa mkombozi mkubwa kutokana na kuweza kuwasaidia wanafunzi zaidi ya 1600 waliokuwa wanakabiliwa na chanagamoto ya kusoma katika mlundikano mkubwa na baadhi yao walikuwa wanakaa chini ya sakafu.
Naye Afisa elimu wa shule za msingi katika halmashauri ya mji Kibaha Maajabu Nkanyemka amesema kwamba kwa sasa hawana mapungufu yoyote ya madawati hivyo hakutakuwa na changamoto ya mwanafunzi wake kujisomea wakiwa wamekaa chini ya sakafu.
MADAWATI hayo 537 ambayo yametolewa na ofisi ya Mbunge wa Kibaha Mji yamegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 yatasambazwa katika kata zote 14 ambapo pia yataweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondolea adha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto hiyo kwa kipindi cha muda mrefu na hatimaye kuongeza kiwango cha ufaulu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.