Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju amesema Rais John Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar ukiwamo uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20.
Hii
ni kauli ya pili kutolewa ndani ya wiki moja ikieleza hali hiyo, baada
ya ile ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Luvuba
aliyoitoa wiki iliyopita baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli,
Ikulu, Dar es Salaam.
Akizungumza
bungeni juzi, Masaju alisema: “Katiba ya Zanzibar si ya Muungano,
masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na ndiyo sababu ulinzi
umeimarishwa visiwani humo kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama.
Alitoa
kauli hiyo juzi jioni wakati akifafanua mambo mbalimbali
yaliyozungumzwa na wabunge wakati wa mjadala wa mwongozo wa mpango wa
Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17 na Mapendekezo ya Mpango
wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
Tangu
kuibuka kwa mgogoro Zanzibar watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakisema
mwarobaini wa mgogoro huo kwa kutumia jitihada za ndani, ufanywe na Rais
Magufuli baada ya jitihada za viongozi wa kisiasa visiwani kukwama.
Mgogoro
huo, ambao umekuwa kawaida kuibuka kila baada ya Uchaguzi Mkuu,
uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum
Jecha kufuta matokeo Oktoba 28 na baadaye kuuitisha upya, kitendo
ambacho CUF inakipinga.
Tangu
wakati huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, Rais wa
Zanzibar, Dk Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd
na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na
Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo ambayo hayakuzaa muafaka.
“Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Serikali mbili.
Hizi Serikali uwepo wake ni Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.
Ukisoma Ibara ya nne ya Katiba si tu kwamba inaweka mgawanyo wa madaraka
katika mihimili mitatu ya Dola, bali inaweka mgawanyo wa madaraka kati
ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.”
Ibara
ya 4 ya Katiba inasema (1) Shughuli zote za Mamlaka ya nchi katika
Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye
mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutekeleza utoaji
haki na pia vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma.
(2)
Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, vyombo vyenye mamlaka ya
kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni Idara ya Mahakama ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano na Idara ya Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia
utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la
Wawakilishi.
(3)
Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya
Muungano, na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo
baina ya vyombo vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya
Muungano kama alivyoorodheshwa katika nyongeza ya Kwanza iliyoko
mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano
ambayo ni mambo mengine yote yasiyo ya Muungano.
(4)
Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza
majukumu yake kwa kufuata masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii.
Masaju alisema Katiba ya Zanzibar ndio inayozaa ZEC.
“Kile
ambacho baadhi ya wabunge wamekisema hapa ni kama kuitaka Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia mamlaka ya Zanzibar na tafsiri
yake ni kama unataka kuleta hoja ya kujenga Serikali moja,” alisema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.