ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 16, 2015

MWANZA YAIADHIBU MOROGORO AIRTEL RISING STARS

Mchezaji wa timu ya  Kinondoni Seleman Mbwezi (Kulia) akijaribu kumtoka mchezaji wa timu ya Morogoro Nickson Kibabage katika mechi ya Airtel Rising Stars iliyochezwa  jana katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume. Morogoro ilishinda 2-1 
Mchezaji wa timu ya Morogoro Richard Wiliam (kulia) akiwania mpira na mchezaji wa timu ya Kinondoni Selemani Bwenzi  katika mechi ya Airtel Rising Stars iliyochezwa  jana katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume. Morogoro ilishinda 2-1.
Mchezaji wa timu ya Morogoro Evidence Kilongozi (Kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa timu ya Kinondoni Frank Kamani katika mechi ya Airtel Rising Stars iliyochezwa  jana katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume. Morogoro ilishinda 2-1. 
Mwanza yaiadhibu Morogoro Airtel Rising Stars
Patashika ya michuano ya vijana chinia ya miaka 12 ya Airtel Rising Stars ngazi ya taifa, jana iliendelea kutimua vumbi katika dimba la Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, ambapo timu za Temeke na Mwanza zilipepetana kwa upande wa wasichana huku Mwanza na Morogoro walitifuana vikali kwa upande wa wavulana.

Kwa kuanzia na mchezo ambao ulizikutanisha timu za wavulana, Mwanza waliwasambaratisha vibaya  Morogoro kwa kuwashindilia magoli 3-1.

Mwanza ambao walionekana kutakata kila idara, walijipatia bao la uongozi mnamo dakika ya 30 kupitia Lazaro Richard, baada ya kuitokea pasi nzuri iliyopigwa na David Richard na kumchambua vizuri kipa wa Morogoro kisha kuukwamisha mpira huo kimiani.

Morogoro ambao katika mchezo wa Jumatatu  wiki hii, waliitandika Kinondoni mabao 2-1, waliamka kutoka usingizi na kufanya mashambulizi kadhaa ambayo hata hivyo hayakuzaa matunda.

Alikuwa ni David Richard ambaye aliandikia Mwanza bao la pili mnamo dakika ya 54, kutokana na krosi safi iliyochongwa kutoka mashariki mwa uwanja na kuusindikiza kwa uzuri kabisa mpira huo langoni mwa Morogoro.

Baada ya goli hilo, Morogoro waliamka na kupeleka mashambuliza ya mara kwa mara langoni mwa Mwanza, na ndipo mshambuliaji wao hatari Evidence Kiongozi alipofunga goli dakika ya 63 na kuamsha matumaini ya walau kusawazisha na hatimaye kutafuta goli la ushindi.

Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa upande wa Morogoro, baada ya David Richard kwa mara nyingine tena, kuifungia Mwanza bao la tatu na mwisho katika mchezo huo mnamo dakika ya 68 na kuhitimisha karamu ya magoli kwa upande wa timu yake.

Katika mchezo mwingine, wasichana wa Temeke waliwaadabisha vikali Mwanza kwa kuwafumua magoli 3-0.

Temeke ambao katika mchezo wao wa kwanza walitaoa kipigo cha mbwa mwizi cha magoli 8-0 dhdi ya Arusha, walianza kupata bao mnamo dakika ya 11 baada ya Shamimu Khamisi kufunga goli maridhawa, baada ya kutokea rapsha langoni mwa Mwanza na kuipa timu yake goli la uongozi.

Iliwachukua takribani dakika takraibani 28, Temeke wakapata bao la pili kupitia kwa Rose Mpoma baada ya kuachia shuti kali la mbali na kuzama moja kwa moja wavuni, na kumwacha mlinda mlango wa Mwanza asijue la kufanya langoni mwake.

Mpaka timu hizo zinakwenda mapumzikoni, Temeke walikuwa mbele kwa magoli 2-0.

Temeke waliendeleza kilio kwa wapinzani wao, katika kipindi cha pili kwa kushindilia msumari wa tatu na wa mwisho mnamo dakika ya 56, baada ya Oppah Masoud kugongeana mpira vizuri na Rose Mpoma na hatimaye kuusukumiza moja kwa moja mpira kimiani.

Baada ya kupata goli la tatu, Temeke walionekana kuridhika na kucheza kwa kijiamini huku wakisubiri kipenga cha mwisho cha mwamuzi,  huku wakiwa wamejikunyajia pointi tatu kibindoni.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.