ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, June 2, 2014

YULE MTOTO ALIYEWEKWA KWENYE BOX MIAKA MINNE AFARIKI DUNIA!

 MTOTO Nasra Said aliyekuwa akiishi kwenye box kwa miaka minne akidaiwa kuteswa na mama yake mkubwa baada ya mama yake kufariki, huku akikosa uangalizi wa karibu, chakula, tiba na huduma nyingine muhimu AFARIKI DUNIA katika Hospitali ya Taifa MUHIMBILI usiku wa kuamkia JANA majira ya saa saba, tatizo ni Nimonia na homa ilipanda sana.
R.I.P NASRA wewe mbele sisi nyuma tutakufuata, Tulikupenda lakini Mungu amekupenda zaidi.
GAZETI LA MWANANCHI LINAANDIKA
WATAFITI wa masuala ya haki za binadamu wamefanya utafiti na kutoa taarifa kwamba wapo watoto magerezani wanaochanganywa na watu wazima, hivyo kuainisha kuwa hayo ni mateso makubwa kwa watoto kisaikolojia na kimakuzi.
Sheria zinaruhusu watoto watukutu kuwekwa kifungoni, ila si kwa lengo la kuwapa adhabu, bali kuwapa mafunzo, lakini inapofikia hatua ya kuwekwa na watu wazima ambao wengi wao huwa wana makosa makubwa na tabia za ajabu, si jambo zuri kwa watoto.
Watoto wote wanahitaji ulinzi, kufundishwa maadili na kupewa makuzi mazuri yasiyo na misukosuko kama ile ya gerezani, kwani hata jela za watoto programu zake ni tofauti na zile za watu wazima.
Wakati wafungwa watu wazima wanapofanyishwa kazi kama vile za mashambani, ujenzi wa barabara, uchimbaji mawe na nyinginezo ngumu, watoto wanapaswa wapewe kazi ndogondogo kama vile za usafi na baadaye wawekewe walimu kwa ajili ya kuwapa elimu kwa mujibu wa viwango vyao vya ufahamu, ili hata wakitoka jela, wasiwe wameachwa mbali na wenzao waliokuwa shuleni.
Watoto wakiwa kifungoni na wakipewa mafunzo mema, wengi wao hubadilika kwa sababu tayari wameonyeshwa mwanga na pengine ni mazingira ndiyo yaliyosababisha wao kuwa watukutu, hivyo jamii inapaswa kuwapa mazingira mengine mazuri ya kujifunza na wala si ya kuwaumiza kisaikolojia na hata kuwapa madhara ya kimaumbile.
Uwepo utaratibu wa kuwatenga watoto na watu wazima katika maeneo kama ya jela, ambayo kimsingi kwanza mtoto si pahali pake, kwake yeye ni nyumbani ambako tunatarajia kuwa ndiko atakakopatiwa malezi, ikiwa itabidi awekwe mbali na wazazi/walezi wake, basi awekwe katika mazingira rafiki kwa afya yake ya kiakili na kimwili.
Yameibuliwa mengi, na mengine ya kutisha bila shaka hayakutajwa katika utafiti, sisi tunaungana na Tume ya Haki za Binadamu kuishauri serikali kuweka sehemu tofauti kwa kinamama wenye watoto wadogo ikiwa mama hao watakutwa na kadhia zitakazowalazimisha wawekwe kifungoni au kizuizini.
Jambo hilo kwa kawaida halihitaji hata kutungiwa sheria, bali dhamira tu ya kibinadamu inabidi itusute na kuona kuwa watoto hawastahili kuishi katika mazingira hatarishi. Mambo kama haya kwa kweli si ya kuyafumbia macho, na tunatarajia kuwa serikali yetu sikivu itakuwa imeyasikia na kudhamiria kuyafanyia kazi kwani ni wazi kuwa watoto hawa watakapomaliza kifungo chao, kuja kuwa raia wema katika jamii itakuwa ngumu kama ngamia kupita katika tundu ya sindano.
Tulidhani hili Serikali inaliona na haikupaswa isubiri iumbuliwe na utafiti, wakati sasa umefika wa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa jela za watoto na sehemu za kuwaweka wanawake wenye watoto wanapokumbwa na mkono wa sheria.
Sababu za kuwa Serikali haina fedha, si sababu za kuridhisha, kwani vipo vipaumbele vingine vya Serikali ambavyo hupatiwa fedha kwa udi na ubani, hivyo hili la watoto nalo la kuwapatia mazingira salama, inabidi tuliweke katika vipaumbele vyetu vinavyochukua nafasi ya kwanza.
Tume ya Haki za Binadamu imefanya kazi yake ya kuibua madhila ya ukandamizaji wa haki za watoto katika jamii, sasa kazi iliyosalia ni ya serikali na jamii kwa upana wake, wakati umefika wa kulivalia njuga suala hili, kwa pamoja tupinge unyanyasaji huu mkubwa kwa watoto kwani ni aibu kwa taifa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.