SHIRIKA la watoto la New Light Children Center Organization
(NELICO) la mkoani Geita kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya jamii Geita,
limeambatana na wawakilishi 20 toka Mabaraza ya watoto ya kata kumi na moja
(11) za wilaya ya Geita kwa ziara ya kimafunzo katika shirika la kutetea Haki
za Wanawake na wasichana, KIVULINI la mkoani Mwanza.
Ziara hiyo ya kimafunzo katika shirika la KIVULINI
imefanyika hapo jana ikiwa na lengo la kujifunza namna KIVULINI ilivyosaidia
Baraza la watoto Mwanza kuweza kuratibu na kutekeleza shughuli zake kikamilifu
na kuwa imara zaidi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa NELICO Bi.
Paulina Alex alisema kwamba ziara hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa mabaraza ya
watoto wilayani Geita juu ya mbinu za kuratibu na kutekeleza miradi mbalimbali
lakini pia kujua mafanikio na changamoto za shirika la KIVULINI katika kupiga
vita ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika mikoa ya kanda ya ziwa.
“Mabaraza ya watoto ya Geita bado ni machanga sana na
hivyo kufanya safari hii ya mafunzo kuwa ya muhimu sana. Katika safari hii
wawakilishi wa mabaraza ya watoto wameweza kupata elimu kubwa kutoka KIVULINI
na Baraza la watoto la Mwanza (Mwanza Youth and Children Network) ambalo ni zao
la KIVULINI” alisema Bi. Paulina.
Ziara hiyo pia ilikuwa na Bw. Maximillian Kitigwa amabe ni
mwakilishi toka shirika la Plan International ambao ni wadau wakubwa wa watoto
kwa mkoa wa Geita pamoja na Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Geita Bi.
Emma Busanji. Watoto hao pia watafanya ziara katika Mkoa wa Arusha kujionea
juhudi za wadau wa maendeleo katika mkoa huo katika kuwaokoa watoto dhidi
ya kufanyishwa kazi hatarishi hasa katika sekta ya madini.
Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea na
kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shirika la Kivulini linahamasisha jamii
(Wanawake, Wanaume na Vijana) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana
kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo
jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.