ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 12, 2013

WATOTO WANNE WA FAMILIA MOJA WAFARIKI DUNIA BAADA YA KULA CHAKULA CHENYE SUMU

Na Nathan Mtega,Namtumbo
WATOTO wanne wa familia moja wa kijiji cha Ligunga kata ya Lusewa tarafa ya Sasawala wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma   wamefariki dunia na wengine 12 wamelazwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoan wa Ruvuma  na wengine katika kituo cha Afya cha Lusewa kwa madai ya kula chakula kilichokuwa na sumu.
 Akiongea na waandishi wa habari katibu tarafa wa Sasawala Fred Maliyao amesema kuwa wanafamilia hao walikula vyakula tofauti  vya aina tatu na walikuwa 19 ambapo chakula kingine kilisadikika kuwa kilikuwa na sumu ambayo iliweza kuwadhuru na kusababisha vifo hivyo.
 Akifafanua Maliyao alisema kuwa katika siku ya sikukuu ya IDD EL FITRI wanafamilia hao walikula ugali kwa mboga ya samaki ,mbonga za majani aina ya chaina na utumbo wa kuku ambao unasadikika ulikuwa umechemshiwa mchuzi wa samaki huku wengine wakila ugali kwa mboga ya mbaazi  na utumbo wa kuku.
 Alisema kuwa walikula chakula kwenye familia baba yao mdogo na mkubwa  kwa nyakati tofauti  ambapo walikuwa wakiifurahia sikukuu ya IDD EL FITR kwenye familia hizo pamoja na kutembeleana na kufarijiana kwa ajili ya sikukuu.
 Kwa upande wake mwanafamilia Bilahi Mumba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 8 mwaka huu majira ya saa 5 hadi saa sita mchana baada ya watoto hao kula chakula kwa Baba yao mdogo Mumba ambaye anadai kuwa alinunua samaki hao kwa mtu mmoja katika eneo la Lusewa kwa bei ya shilingi 1500.
 Mumba aliiwataja watoto hao waliofariki kuwa ni Zidane Mumba[2.5] Tazamio Mumba [9] Selemani Mumba [7] na Zahara Mumba [2] na kuwa wote ni wa familia moja.
 Naye Muuguzi wa kituo cha afya cha Lusewa Edrisa Ndauka alisema kuwa walipokelewa wagonjwa 16 kituoni hapo na wanne walifariki dunia huku watano walikimbizwa hospitali ya rufaa ya  mkoa wa Ruvuma mjini Songea na wengine walibaki kituoni hapo.
 Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Abdula Lutavi baada ya kushudia na kuwafariji wanafamilia waliokumbwa na mkasa huo hilo alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa kwa kuwa walioathirika ni watoto wa familia moja.
 Lutavi alisema licha ya watalamu kuchukua matapishi na mabaki ya vyakula hivyo kwa kwenda kuvipima lakini taarifa za awali zinaonyesha kuwa sumu iliwekwa kwenye samaki  maana wote waliogusa samaki au mchuzi wake wamepata athari.
 Mkuu huyo ametoa onyo  kwa baadhi ya watu wa kijiji hicho  ambao huvua samaki kwa kutumia sumu mbalimbali zikiwemo za zao la Tumbaku kwa ajili ya kujipatia kitoweo waache mchezo huo badala yake watumie vifaa vya kisasa zaidi.
 Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Deusdedit Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wanamshikilia mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Salumu kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.
 Naye Mganga Mkuu mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Ruvuma Benedict Ngaiza amethibitisha kupokea wagonjwa sita waliofikishwa hospitalini hapo baada ya tukio hilo hali zao zinaendeleavizuri na uchunguzi zaidi unaendelea kutambua sumu inayodaiwa kuleta madhara hayo kwa familia hizo.

Kwa hisani ya demashonews.blogspot.com

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.