ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 23, 2013

MAONI YA MH. LOWASSA KWA TUME YA KATIBA MPYA

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiongozana na Katibu Mkuu Mstaafu wa uliokuwa Umoja wa Nchi huru za Kiafrika (OAU),Dr. Salim Ahmed Salim ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, mara baada ya Mh. Lowassa kutoa maonai yake mbele ya tume hiyo.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kukusanya Maoni ya Katiba mpya,mara baada ya kutoa maoni yake.

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akipongezwa na Mjumbe wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya,Dk. Senkondo Mvungi mara baada ya kutoa Maoni yake.


YAFUATAYO NI SEHEMU YA MAONI ALIYOYATOA MH. EDWARD LOWASAA:

Kwanza ningependa kukupongeza wewe mwenyekiti Mh Jaji Warioba pamoja na tume nzima kwa imani kubwa ambayo Rais ameionesha kwenu, ni kwa kuwapa jukumu hilo zito na muhimu kwa nchi yetu.

Wananchi pia wamekuwa na imani kubwa na wamejenga matumaini ya kila kitu kwa tume hii. Kutokana na hilo wamekuwa wakitoa maoni ambayo mengine hayahusiani na katiba, yaani siyo ya kikatiba.Pengine na mimi nitakuwa miongoni mwao, kwa hiyo naomba radhi mapema, iwapo maoni yangu haya mengine , yataonekana si ya kikatiba.

Katiba yetu ya sasa ni nzuri, imetuongoza katika umoja na mshikamano wa kitaifa kwa muda wote huo.Lakini, kutokana na hali ya dunia ya sasa, ni vyema kuwepo na katiba mpya ili kuendana na hali halisi.

Kuna mambo manne ambayo kwa imani na mtizamo wangu ningependa yawemo katika katiba yetu ijayo.

1.ELIMU BURE

Moja ya haki za mtoto ni kupata elimu. Ningependa suala la elimu bure ya sekondari liwemo kwenye katiba yetu. Katiba itamke wazi kuwa elimu ya sekondari ni bure.Nchi yetu bado ina idadi kubwa ya watu wake ambao ni masikini.

Uwezo wao wa kipato ni mdogo.Naamini kabisa hili linawezekana na serikali inaweza kugharimia elimu ya sekondari ikawa bure. Hii itatoa nafasi ya kujenga taifa lijalo lenye idadi kubwa ya vijana watakaokuwa wamepata elimu ya sekondari.Wabunge wenzangu bila shaka wanalijua hili.

Ukweli katika majimbo yetu wazazi wamekuwa wakishindwa kulipia karo ya shule kwa  watoto wao. Wabunge tumekuwa tukibeba mzigo huo japo kidogo. Kwa hiyo, kifungu cha ELIMU BURE KWA SEKONDARI, kiwepo kwenye katiba.

2.ADHABU YA KIFO-DEATH PENALT

Katiba ya sasa haisemi wazi kuhusu adhabu ya kifo.Inazungumzia tu haki ya uhai.Ibara ya 14 ya katiba hii ya jamuhuri ya muungano wa tanzania ya mwaka 1977 inatamka kiujumla tu kuwa KILA MTU ANA HAKI YA KUISHI NA UHAI WAKE KULINDWA.

Lakini , haki hiyo inanyang'anywa na kifungu nambari 196 cha sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16(penal code ,cap 16), kinachotamka kuwa adhabu ya kifo(death penalty or capital punishment) kwa kosa la mauaji ya kukusudia.

Adhabu hiyo hiyo pia utolewa kwa kosa la uhaini.Sasa mapendekezo yangu mimi ni kwamba kuwe na ibara katika katiba mpya inayotamka wazi kuwa HAKUTAKUWA NA ADHABU YA KIFO HAPA NCHINI HATA KWA KOSA LA KUKUSUDIA AU UHAINI.

3.MATUMIZI YA FEDHA KATIKA UCHAGUZI

Katika sehemu nyingi hapa nchini mwananchi kama hana fedha hawezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.Katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni.Iainishe ni matumizi gani ya lazima ambayo mgombea hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake, mfano kuwakusanya wapiga kura kwenda kupiga kura gharama hizo nani azibebe.

Katiba ifafanue rushwa ni nini kwenye chaguzi hizi.Au tuwe na mfumo wa PROPORTIONAL REPRESENTATION ,vyama viwe ndiyo vinaingia kwenye chaguzi kuwania majimbo na siyo wanachama,huko kila mtu atakuwa anapigania chama chake kupata kura nyingi ili wapate viti vingi zaidi, pengine hii itasaidia kuondoa kikwazo cha mtu kuwa na uwezo wa kifedha ndiyo aweze kuwania uongozi.

4.ARDHI

Kwa mwanadamu, kunyang'anywa haki ya kutumia ardhi ya nchi aliyozaliwa ni sawa na kunyanng'anywa haki ya uraia wake. Katiba hii ya sasa inawapa nguvu wakulima katika suala la ardhi, na kuwasahau wafugaji.

Wafugaji wamekuwa wakimbizi katika nchi yao, wamekuwa wakitangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao, ile ardhi waliyokuwa wanaimiliki wakiondoka kutafuta malisho huku nyuma imekuwa ikimilikishwa watu wengine, wakulima au wawekezaji, hili kwakweli si jambo jema .

Tumeshuhudia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.Kwa hiyo, mimi ningependa katiba hii mpya impe mfugaji haki katika suala la ardhi kama.Ardhi ya wafugaji ilindwe, ifafanuliwe kikatiba haki yao hiyo. Kuwe na hali ya 50,50 situation kati ya mfugaji na mkulima katika suala zima la umiliki wa ardhi,kikatiba!

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.