Jesus Christ Superstar … Carl Anderson as Judas in the 1973 film version. Photograph: Ronald Grant Archive |
Anna Mghwira
Kwa takiribani miaka 2000 sasa Waumini wa dini ya Kikristo
huadhimisha sikukuu hii ya Krismas ulimwenguni kote. Krismas ni tafsiri fupi ya
siku ya kuzaliwa Kristo. Kristo mwenyewe hakuwa Mkristo kwa maana kuwa jina
Kristo lilipatikana kwa ujio na mauti yake. Yeye alikua Myahudi wa dini ya
Kiyahudi.
Tarehe hasa ya kuzaliwa Kristo haifahamiki ijapo majira
yanafahamika na yanatofautiana kati ya desturi mbalimbali za Kikristo. Kwa
mfano nchi za magharibi ndizo zinazoadhimisha tarehe 25 Decemba kama siku ya
kukumbuka kuzaliwa kwa Kristo Yesu. Desturi ya magharibi inafuata tarehe
iliyoandikwa mwaka wa 336 baada ya kuzaliwa Kristo.
Desturi zingine za Kikristo huadhimisha siku hii na kuipa maana
tofauti, kwa mfano desturi ya Kiothodox huweka mkazo zaidi katika majira ya
kuzaliwa Kristo (epiphany) kuliko siku yenyewe ya kuzaliwa. Hawa pia huhesabu
mwaka wao mpya tofauti na mwaka wa kalenda tunaotumia unaotokana na desturi za
magharibi. Wao huadhimisha siku za majira ya mwaka mpya mwezi wa nne wa kila
mwaka.
Aidha kuna tafsiri mbalimbali juu ya ujio na utambulisho wa
Kristo. Kwa jinsi ya desturi za Kiyahudi, alikozaliwa Yesu na ambalo ndilo
taifa lake la asili, Kristo yaani Masihi bado hajaja kwa maana kwao masihi ni
mfalme wa aina ya kidunia.
Yaani ataonekana kwa macho kama mfalme na si kama alama ya
imani. Na si kama mwana wa Mungu kama imani ya Kikristo inavyoelekeza. Baadhi
ya Wayahudi pia hawamtambui Yesu kama masihi mpaka leo. Kwa hiyo Kristo wa
imani na Kristo wa matendo wanaweza kuwa viumbe viwili tofauti.
Kwa jinsi hii maana ya Krismas inatofautina katika misingi hii.
Na kwa sababu hii tafisiri mbalimbali za maana ya Kristo huelekezwa katika
maana ya ujio wa Kristo zaidi kuliko katika hali ya kimwili ya kuwa mwana wa
Yusufu na Maria.
Kwa hiyo Wakristo huadhimisha siku hii kama ishara ya ujio wa
mkombozi wa kiimani zaidi. Maana ya ukombozi wenyewe nayo hutofautiana, wengine
wakimtazama Yesu kama Mungu aliyefanyika mwanadamu, wengine wakimtazama
kifalsafa na kumpa maana kubwa ya mafunzo ya uadilifu ambayo wakristo wanapaswa
kufuata.
Katika mkazo wa mafundisho, kuna mambo mengi yanayohusishwa na
ujio wa Kristo ulimwenguni. Tafsiri nyingi zimetawaliwa na desturi za magharibi
ambazo kwa kweli hazina uasili na ujio wa Kristo, lakini kama ilivyo katika
masuala mengine ya jamii, jamii za awali za magharibi zinaonekana katika
historia ya binadamu kuwa na mwamko wa kuchukua mambo na kuyafanyia kazi kwa
haraka kuliko jamii zingine na kwa hiyo zinamiliki tafisri za mambo mengi hata
yale yasiyokuwa na asili yao.
Kwa hili hatuwezi kuzilaumu jamii hizi au watu binafsi kwa
juhudi zao. Tunaweza badala yake kutoa changamoto kwa jamii zingine ulimwenguni
na hasa za Afrika ambazo zimekuwa nyuma sana katika kuweka mambo yake katika
historia ya ulimwengu na hata kwa mambo yake yenyewe.
Kwa sababu hii tafisri kuu ya kile kinachoitwa Ukristo kwa
sehemu kubwa ni desturi ya magharibi na tafsiri yao juu ya dini hii. Ni kwa
sehemu inafanana na Uislamu pia ambao una destri kuu ya Kiarabu. Kwa hiyo kwa
mfano vita kuu ya maneno na ya silaha kati ya Waarabu na Wazungu ina msingi
katika dini zao.
Tukio la septemba 11 la mwaka 2001 lilihitimisha kwa sehemu
ugomvi mkali kati ya desturi hizi mbili na mpaka sasa vita vya mashariki ya
kati vinajengwa katika msingi wa imani na mali – mafuta kwa upande wa Waarabu
na matumizi ya mafuta kwa upande wa Wazungu.
Desturi hizi mbili zinawagusa na kuwaathiri Waafrika kwa namna
ambayo si rahisi kujitoa katika makucha ya mabwana hawa wawili: Mzungu na
Mwarabu. Kwa hiyo kama kuna ukombozi Mwafrika anahitaji ni kujitoa katika
makucha ya hawa kwanza, hata katika tafisri za kiimani.
Kisha kuangalia alikotoka na anakotaka kwenda na atakavyokwenda.
Bila ya hivyo ukombozi wa Kikristo unaweza kubaki kuwa ukombozi wa kujua mila
na desturi za watu wengine na imani zao, na kamwe usimkomboe Mwafrika. Hili ni
kweli ikizingatiwa kuwa ukoloni ulikuja na Ukristo na utumwa ulikuja na Uislam!
Tunahitaji kutafakari na kuchukua hatua mapema!
Nitoe mfano wa desturi ya Wakristo kusali wakifumba macho. Utani
unakuja kuwa kwa kufundishwa kufumba macho Mwafrika alifumbia macho mambo ya
msingi kama rasilimali zake na wakati angali amefunba macho, mzungu akachukua
kisha akamtawala!
Kuna ukweli kuwa mila na desturi za Kiafrika hazikuwa na utamaduni wa kufumba macho wakati wa kusali. Makabila yetu mbalimbali huendesha
ibada za kimila nuruni, katika mwanga ambapo kila mtu anamwona mwenzake. Aidha
dini za asili kadhaa huamini na kuapa kwa jua na mwezi, kwa hiyo kufumba macho
hakupo!
Nimewahi kushuhudia mwinjilisti mmoja ambaye alifungua macho
wakati wa sala akakuta paka anataka kuchukua samaki waliokuwa wametengwa mezani
na bila kujali imani yake na ya kuwa yeye ni kiongozi wa dini, alipoona paka
ananyemelea samaki alipiga kelele “ paka anachukua samaki” kwa lugha ya kimila
aliyotumia alisema”nyau ahora somba nye”!
Yaani paka anachukua samaki wakati wengine wamefunga macho
wakisalia chakula!. Tukio hili lilinifanya nitafakari sana kama kweli imani hii
inatokana na kufunga macho ama inatakiwa itokane na kufunga rohoni zaidi ili
mtu astahimili kuyafumbia macho mambo ya dunia hii yanayopotosha!
Huu ni upande mmoja wa shilingi, upande wa pili ni kuwa wakoloni
Wakristo walipofika na kufundisha kufumba macho ya akili wakati wao wakifumbua
na kutumbua, ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo na leo ni vigumu sana kuwatoa
katika fahamu zetu, katika mipango ya kujiendeleza na kujikwamua na udhalimu
waliouanzisha.
Sheria zetu na umahiri wake msingi wake si zetu kwa kweli, ni
mambo ya kuiga na kuigiza! Mwafrika hana desturi ya kumweka mkosaji kizimbani,
kumhoji maswali akiwa ametengwa na jamii aliyoikosea. Mwafrika wa asili
alitumia njia za matambiko kubaini wakosaji, kisha kuwarejesha ama kuwatenga
kwa kuwapeleka mbali na makazi asili ili hayamkini wajifunze na kurejea tabia
ya utu.
Tunahitaji kubadilika! Tunahitaji kufanya kazi ya ziada
kujua asili yetu na kuirejesha! Wakati mwingine nimefikiri kuwa pengine
turudishe utumwa tena wa jinsi yetu ili hatimae tujikomboe.
Mtihani mkubwa wa imani upo hapo: katika kuyaona mambo mabaya
yanayofanywa duniani na yenye mvuto machoni kama vile yanafaa lakini kumbe
ndiyo yanayotuangamiza.
Kuzaliwa kwa Kristo ni wito kwa Wakristo kuleta amani, upendo na
nuru katika ulimwengu. Ni tafsiri nzuri hata kama haitokani na desturi ambayo
ningeitaka. Kwa makala hii niwatakie wasomaji wetu Siku kuu njema na niwape
mtihani kufikiri kama masihi angetoka afrika angefananaje na ujumbe wake
ungekuwa nini??
Kama masihi huyu angezaliwa leo Tanzania angekuwa na sura na
umbo gani?
Angewakilisha kundi gani?
Angeongea lugha gani?
Angekuwa na imani
gani na angejishughulisha na nini?
Kristo alikuja ili wawe na uzima kisha wawe nao tele. Je tunao
uzima huo?
Yaani maisha bora ya kujitosheleza kusherehekea siku kuu hii na
zingine zijazo na tunazoweza kuvumbua?
Mungu atubariki tunapokula na kunywa tusile kama wajinga wasio
na imani bali kama werevu wenye hekima! Heri ya krismas kwenu Nyote!
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.