Matamshi yake katika hotuba kupitia televisheni ya taifa, yamepishana na taarifa za awali kuwa alikuwa akijitayarisha kujiuzulu. Bw Mubarak amesema atakabidhi baadhi ya majukumu kwa makamu wa rais Omar Suleiman, lakini taarifa kamili ya jambo hili haifahamiki vyema.
Maelfu ya waandamanaji katika eneo la wazi la Tahriri wamepokea kwa hasira tangazo lake hilo. Walikuwa wakipiga kelele za "tumechoka na Mubarak", huku waandamanaji wengine 'wakipeperusha' viatu vyao kwa ghadhabu. Maelfu wameripotiwa kutembea kuelekea katika ikulu ya rais ambayo iko umbali mrefu.
WAANDAMANAJI TAHRIR.
Bw Mubarak alikwisha sema mapema kuwa hatogombea urais mwezi Septemba, na kusema atasalia kusimamia mchakato wa mabadiliko ya katiba.
"Natangaza nia yangu ya kuendelea na kuitetea katiba na kuwalinda wananchi na pia mabadiliko kwa yeyote atakayechaguliwa mwezi Septemba katika uchaguzi huru na wa wazi," amesema Mubarak. Akiwahutubia moja kwa moja waandamanaji "waliopo Tahrir na kwingineko" katika kile alichoita "hotuba kutoka moyoni mwake", bw Mubarak,82, amesema: "Sioni aibu kusikiliza vijana wa nchi yangu na kuchukua hatua."
Ameomba radhi kwa familia za waandamanaji waliokufa katika mapigano na majeshi ya usalama katika wiki za hivi karibuni, na kusema waliohusika na vifo hivyo watachukuliwa hatua.
MUBARAK ALIINGIA MADARAKANI BAADA YA ANWAR SADAT KUUAWA.
Bw Mubarak ameongeza kuwa sheria za hali ya dharura nchi humo zitaondolewa pale tu hali itakapokuwa sawa, na kusema atawapuuza "madikteta kutoka nje ya nchi". "Misri imepitia nyakati ngumu na hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea," amesema. "Hasara kwa uchumi wetu itasababisha hao vijana wanaotaka mabadiliko kuwa wa kwanza kuathirika."
OBAMA AMEKUTANA NA MAAFISA WA USALAMA.
Rais wa Marekani Barack Obama amekutana na maafisa wake wa usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani, baada ya hotuba ya Rais Mubarak. Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni, imezidisha wito wake kwa sauti za waandamanaji kusikilizwa.
Mapema, katibu mkuu wa chama kinachotawala cha Bw Mubarak - National Democratic Party - Hossam Badrawi alisema, jambo sahihi kwa rais kufanya ni kuondoka madarakani, na kuwa hakuwa akitarajia Bw Mubarak kuwa bado rais siku ya Ijumaa.
Wakati huohuo, jeshi la Misri limetangaza kuwa liko tayari "kulilinda taifa". Shirika la habari la Misri Mena, limeripoti kuwa baraza kuu la jeshi lipo katika hali ya "kulilinda taifa, na matakwa ya watu".
KWA HISANI YA BBC swahili.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.