ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 14, 2026

MCHUNGAJI ANASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA KUHUSIKA NA MAUAJI YA MKEWE


Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia na linaendelea kumhoji mchungaji wa Kanisa la Habari Njema, Kasese Gervas Bilalo (47), kwa tuhuma za kumuua mke wake, Martha Faustine (45).


Tukio hilo limebainika Mei 12, 2026 majira ya saa 6:00 mchana katika Kijiji cha Nyarututu, Kata ya Bwanga, Wilaya ya Chato, mkoani Geita, ambapo marehemu alikutwa amefariki ndani ya nyumba yao katika mazingira ambayo Jeshi la Polisi limebaini kuwa ni ya kutengenezwa. Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa mtuhumiwa alimvizia mkewe akiwa amelala, kisha akamkaba shingoni kwa kutumia kamba ya katani kabla ya kumning’iniza juu ya kenchi ili tukio hilo lionekane kama kujinyonga.


Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa marehemu alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa na mahusiano ya nje ya ndoa yao, hali iliyosababisha migogoro ya mara kwa mara katika familia hiyo. 


Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya uchunguzi, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kukamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe katika mamlaka husika za kisheria.


Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutumia njia za amani na za kisheria katika kutatua migogoro badala ya kujichukulia sheria mkononi, jambo linaloweza kusababisha madhara makubwa au kupoteza maisha.


Imetolewa na:

SACP Safia Jongo

Kamanda wa Polisi

Mkoa wa Geita

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment