Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania, (TASHICO) imesema ukarabati wa meli kongwe ya abiria na mizigo, MV Liemba, umefikia asilimia 57, huku ikieleza kuwa kukamilika kwake kutaleta mapinduzi ya kiuchumi katika nchi za ukanda wa maziwa makuu.
Akizungumza Mhandisi wa mradi huo Elias Kivara amesema vifaa vyote vinavyotakiwa kukamilisha ukarabati wa meli hiyo tayari vimefika akitaja kuwa kinachoendelea sasa ni kukamilisha zoezi la kupaka rangi na kwamba maboresho ya meli hiyo yataifanya iwe katika hali ya upya na usasa.
“Meli imeboreshwa kutoka ilivyokuwa wakati ule, tumeweka siti za kisasa, kutakuwa na sehemu ya starehe, ambayo inaweza kuchukua watu 53 na vyumba vyote vitakuwa na kiyoyozi, vitu vyote vimewekwa vipya na tumezingatia vifaa vya usalama, vyote vitakuwepo ndani ya meli,"amesema Kivara.
Amesema mpaka sasa wapo wafanyakazi 45 wakiwemo wazawa 43 na kutoka Korea wawili.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TASHICO, Daniel Mwambungu amesema kuwa kati ya jumla ya dola milioni 13, sawa na Sh. bilioni 29 za mradi huo kiasi cha dola milioni 7.8 kimeshalipwa.
Amesema ukarabati wa meli hiyo ulianza Julai 2024 huku ikitarajiwa kuanzia safari za majaribio mnamo mwezi Juni mwaka huu na kuanza safari rasmi mwezi Julai 2026
MV Liemba ilikuwa inafanya kazi zake kuzunguka mwambao wa ziwa Tanganyika ikiwemo Kigoma, Katavi, Rukwa na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mzigo, ilisimama safari zake mwaka 2018 kutokana na uchakavu wa mitambo yake.

Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment