ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, February 10, 2026

ULEGA AWAAGIZA WAKANDARASI: LIPENI WAFANYAKAZI KWA MUJIBU WA SHERIA

 

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewaagiza wakandarasi wote nchini kuhakikisha wanalipa watumishi wao kwa kuzingatia sheria za kazi za Tanzania, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya kuwapunja wafanyakazi.


Waziri Ulega alitoa agizo hilo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Same–Kisiwani–Mkomazi yenye urefu wa kilometa 100.5, mradi unaotekelezwa na mkandarasi M/S China Communication Construction Company Ltd.


Katika ukaguzi huo, Waziri alipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wakidai kuwa wanalipwa mishahara midogo isiyokidhi viwango vya kisheria. Hali hiyo ilimlazimu Waziri Ulega kutoa onyo kali kwa mkandarasi huyo kuhakikisha anarekebisha mara moja dosari hizo.


Ingawa msimamizi wa kampuni hiyo alimwahidi Waziri kuwa suala hilo litafanyiwa kazi, Mbunge wa Mkuranga alisema hatasita kulifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ili wamiliki wa kampuni hiyo waitwe nchini na kupewa maelekezo ya kufuata sheria za Tanzania kuhusu malipo ya wafanyakazi.


Aidha, Waziri Ulega alionesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo ambao ulianza Januari mwaka jana, akisisitiza kuwa ucheleweshaji haukubaliki kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kwa wananchi.


Hata hivyo, aliwahakikishia wananchi wa Same kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaambatana na ujenzi wa vituo pamoja na uwekaji wa taa za barabarani ili kuleta mwanga na kuchochea shughuli za kibiashara katika maeneo hayo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema matarajio makubwa ya wananchi wa Same ni kuona barabara hiyo inakamilika kwa wakati ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo pamoja na Taifa kwa ujumla.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment