
TIMU ya Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa kirafiki asubuhi ya leo kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yamefungwa na mshambuliaji wa Kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube Mpumelelo na beki Aziz Andambwile Mwambalaswa ambaye pia alijifunga kuwapatia bao la kufutia machozi Fountain Gate.
Huo ulikuwa mchezo wa pili wa kujipima kwa Yanga katika maandalizi ya msimu mpya chini ya benchi jipya la Ufundi, baada ya awali kuifunga Rayon Sports ya Rwanda 3-1 wiki iliyopita Jijini Kigali Kigali – mbali na ule ambao walishinda 4-0 dhidi ya wadogo zao, U20 hapo hapo KMC Complex.




Yanga SC inatarajiwa kuuanza msimu kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu, Simba SC Septemba 16 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Lakini Yanga inaweza kuwa na mchezo mwingine mkubwa katika kilele cha Wiki ya Mwananchi Septemba 12 hapo hapo Uwanja wa Mkapa.
Benchi jipya la Ufundi Yanga lipo chini ya Kocha Mkuu, Mfaransa Romain Folz na Msaidizi wake, Mspaniola Alejandro Manu Rodríguez Lázaro na Kocha wa Makipa, Majdi Mnasria.
Wengine ni Mtaalamu wa Viungo (Physiotherapist), Youssef Ammar wote kutoka Tunisia, Kocha wa Physic, Tshephang ‘Chyna’ Mokaila kutoka Botswana, Mchambuzi wa Video, Thula Bantu na Mkurugenzi wa Ufundi, Paul Matthews wote raia wa Afrika Kusini.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment