INEC
yatangaza majimbo mapya ya uchaguzi
Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanzishwa kwa majimbo mapya nane ya
uchaguzi pamoja na kubadilishwa kwa majina ya majimbo mengine 12, ikiwa ni
maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Akitoa
taarifa hiyo leo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo,Jaji wa Mahakama ya
Rufani Jacobs Mwambegele, amesema uamuzi huo umezingatia ongezeko la watu,
ukubwa wa maeneo ya kiutawala, pamoja na mahitaji ya uwakilishi wa karibu zaidi
kati ya wananchi na wawakilishi wao bungeni.
Kwa mujibu
wa Jaji Mwambengele, majimbo mapya yaliyoundwa ni kama ifuatavyo:
- 📌Dar es Salaam:
- Jimbo la Ukonga limegawanywa
na kuanzishwa Jimbo la Kivule
- Jimbo la Mbagala limegawanywa
na kuanzishwa Jimbo la Chamazi
- 📌Mbeya:
- Jimbo la Mbeya Mjini limegawanywa
na kuundwa Jimbo la Uyole
- 📌Dodoma:
- Jimbo la Dodoma Mjini limegawanywa
na kuundwa Jimbo la Mtumba
- 📌Simiyu:
- Jimbo la Bariadi limegawanywa
na kuundwa Jimbo la Bariadi Mjini
- 📌Geita:
- Jimbo la Busanda limegawanywa
na kuanzishwa Jimbo la Katoro
- Jimbo la Chato limegawanywa
na kuundwa Jimbo la Chato Kusini
- 📌Shinyanga:
- Jimbo la Solwa limegawanywa
na kuanzishwa Jimbo la Itwangi
Aidha, Tume
hiyo imesema majina ya majimbo 12 ya uchaguzi yatafanyiwa mabadiliko ili
kuendana na mabadiliko ya kiutawala, kijografia na mahitaji ya kitaifa ya
utawala bora. Orodha kamili ya majimbo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya majina
inatarajiwa kutangazwa rasmi katika tangazo la serikali litakalotolewa hivi
karibuni.
Tume
imewahakikishia Watanzania kuwa mchakato huo umezingatia misingi ya usawa, haki
na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, na unalenga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa
mwaka huu unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia uwakilishi wa kweli wa
wananchi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.