VICTOR MASANGU,MLOGANZILA
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tawi la Mloganzila katika kukabiliana na changamoto ya wimbi la kuwepo kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa ubongo,mishipa ya fahamu na kiharusi imeamua kutoa elimu maalumu kwa wananchi kwa lengo kujikinga na magonjwa hayo.
Hospitali hiyo mbali na kutoa elimu hiyo pia imeweza kutoa huduma mbali mbali za upimaji wa afya wa magonjwa kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila.
Hayo yamebainishwa na Naibu mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila Dkt. Judith Magandi wakati wa maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kiharusi duniani.
Naibu Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuwahimiza wagonjwa wenye changamoto za kiharusi wajitokeze ili waweze kupatiwa tiba sahihi kwa wakati kwa lengo la kuepuka madhara zaidi.
Dkt. Magandi amesema kwamba tatizo la kiharusi ni kubwa na kuongeza kuwa kwa MNH-Mloganzila katika kliniki ya ubongo na mishipa ya fahamu ambapo kwa siku moja wanaona wagonjwa kati ya 140 hadi 170 ambapo kati ya wagonjwa hao asilimia 60 wanabainika kuwa na kiharusi.
“Baada ya kuona ukubwa wa tatizo la kiharusi Muhimbili Mloganzila tumeamua kuboresha huduma za magonjwa ya kiharusi kwa kuanzisha kitengo maalum cha kuhudumia wagonjwa wenye kiharusi ambapo tumeweka vifaa tiba vya kisasa vyenye uwezo wa kufuatilia mwenendo wa mgonjwa kwa wale wagonjwa ambao wamelazwa wodini.
Kwa Upande wake Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu MNH-Mloganzila Dkt. Mohamed Mnacho amesema kuwa ugonjwa wa kiharusi ni moja kati ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo na ulemavu duniani.
Pamoja na hayo, amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 12 duniani wanatatizo la kiharusi ambapo kati ya hao watu milioni 6 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo kwa mwaka.
Aidha ameiomba jamii kuacha kabisa na baadhi ya tabia ambazo zinaweza kuchangia watu kupata ugonjwa wa kiharusi ikiwemo uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, uzito mkubwa pamoja kutokufanya mazoezi.
Nao baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbali mbali ambao wamepatiwa mafunzo ya kujikinga na ugonjwa huo wamesema kwamba elimu waliyoipata kutoka kwa madaktari bingwa itakwenda kuwasaidia.
Siku ya kiharusi Duniani uadhimishwa Oktoba 29 kila mwaka ambapo kwa Muhimbili Mloganzila imeadhimisha siku hiyo kwa kutoa huduma mbalimbali bure ikiwemo upimaji wa shinikizo la damu, elimu ya lishe pamoja na ugonjwa wa kiharusi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.