ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 26, 2024

REA KUENDELEA KUFANYA TAFITI ZA UFANISI WA BIDHAA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (katikati) akizungumza jambo alipotembelea Banda la Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambao ni wazalishaji wa Mkaa Mbadala maarufu kama Rafiki Coal Briquettes. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na watumishi wa REA kwenye Banda la Maonesho la REA katika Tamasha la Kizimkazi linalofanyikia eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko akimkabidhi Cheti Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy cha kutambua mchango wa REA kwenye Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililofanyikia eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Na Mohamed Saif, Zanzibar

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema Wakala utaendelea kufanya tafiti za bidhaa za Nishati Safi za Kupikia ili kubaini ufanisi wa teknolojia zinazosambazwa kwa wananchi.

Mhandisi Saidy amesema hayo Agosti 23, 2024 alipotembelea Banda la Wakala katika Tamasha la Kizimkazi eneo la Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

"Tutaendelea kufanya utafiti wa bidhaa mbalimbali za Nishati Safi za Kupikia ili kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Nishati Safi ya Kupikia kwa wote inapatikana kwa gharama nafuu na yenye ufanisi," amesema.

Amesema lengo ni kuwa na teknolojia sahihi, rafiki na yenye gharama nafuu ili kumuwezesha na kumrahisishia kila Mwananchi kuwa na bidhaa bora kama ilivyo dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusiana na matumizi ya Nishati safi ya Kupikia kwa wote.

"Tutahakikisha lengo la Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 la kufikisha asilimia 80 ya wananchi wanaotumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034 linafikiwa," amesema.

Mhandisi Saidy vilevile alitembelea mabanda ya Wadau mbalimbali wanaojihusisha na uandaaji, uuzaji na usambazaji wa Nishati Safi ya Kupikia na kujadiliana masuala mbalimbali hususan namna bora ya kuendelea kuboresha bidhaa zao ili kuleta tija inayokusudiwa.

Awali kabla ya kutembelea  Maonesho ya Kizimkazi, Mhandisi Saidy alishiriki Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililoandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na Benki ya Uwekezaji ya Tanzania (TIB) kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Taasisi zake ikiwemo REA ambapo Wakala ulipata fursa ya kuelezea suala la Upatikanaji wa Fedha katika kuendeleza Nishati Safi ya Kupikia.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.