Afisa
Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)
Amina Miruko akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maonyesho hayo |
Baraka Mashauri ni Afisa kutoka Shirika la Wakati wa Meli Tanzania (TASAC) akizungumza wakati wa maonyesho hayo |
NA OSCAR ASSENGA, TANGA
SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa Wakuu wa wilaya za Mkoa wa Tanga na viongozi wa Vijiji kutokuvipokea vyombo vya majini ambavyo havijakidhi vigezo vya kisheria katika maeneo yao kupakia abiria ili nao waweze kuwa sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanaokoa maisha ya abiria.
Lakini pia kuwa sehemu ya kuhakikisha nao washiriki kudhibiti safari zinazofanywa na vyombo vinavyotumika kubeba mizigo kupakia abiria na hivyo kuvunja sheria jambo ambalo linahatarisha maisha.
Wito huo ulitolewa leo na Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Tanga Captain Christopher Shalua wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maonyesho ya 9 ya biashara na Utalii yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwahako Jijini Tanga.
Alisema iwapo viongozi hao watashiriki kwenye suala hilo itakuwa ni mwarobaini wa kuweza kudhibiti vyombo ambavyo havijaruhusiwa kisheria kufanya shughuli za kubeba abiria na hivyo kuondokana na matukio mbalimbali yanayoweza kujitokeza ikiwemo ajali za majini.
“Lakini pia niwaambie sisi kama Shirika Kabla hatujachukua sheria inabidi tuwaelemishe watu hivyo tumejitahidi sana kutoa elimu kwa maeneo sugu ya watu wanaosafiri kupitia majahazi katika maeneo ya Mkwaja,Kipumbwi na Pangani kwa wamiliki na manahoida wa vyombo”Alisema
Alisema kubwa zaidi ni wao kutambua kwamba wana wajibu wa kuhakiksiha hawavunji sheria na kuhatarisha usalama wa watu wanaotumia vyombo hivyo kwa sababu havijakidhi vigezo ambavyo vinatakiwa kubeba abiria.
“Tumekuwa tukiwasiliana na Taasisi za Serikali ikiwemo viongozi wa Vijiji,Wakuu wa wilaya,Wakuu wa Polisi wilaya na Mkuu wa Mkoa kumpeleka barua kuwataarifu shughuli zinazofanyika maeneo hayo sio halali na zinahatarisha maisha ya abiria na hatua zinazofuata ni kuchukua hatua za kisheria”Alisema
Captain Shalua alisema kwa sababu wanapopewa leseni zinakuwa na masharti kwamba chombo chako ni cha mizigo na hakiruhusiwi kubeba abiria hivyo wanapovunja sheria wanachukuliwa hatua kali ikiwemo kutozwa faini na kuwapeleka mahakamani au vyote viwili kwa pamoja .
“Kama unavyofahamu eneo la Mwambao wa Bandari ya Tanga ni kubwa sana na tunategemea viongozi wa serikali za vijiji tusaidiana nasi kuweza kudhibiti suala hilo kusimamia usalama “Alisema
Hata hivyo alisema wamiliki wa vyombo vya majini na waendesha vyombo hivyo wanapaswa kuzingatia masharti ya leseni yao kwa wasafiri kwa kuwaeleza kwamba hawatakiwi kupanda kwenye majahazi ya mizigo kwa sababu hakuna mtu anayewalazimisha .
“Hivyo wakipata uelewa kuhusu madhara yake watafanya maamuzi sahihi ya kuttokupanda vyombo hivyo na hivyo kusaidia kwa asilimia kubwa kuondokana na changamoto ambazo wanazoweza kukumbana nazo wawapo safarini”Alisema
Captain Shalua pia alisisitiza umuhimu wa vyombo hivyo kwa na vifaa vya kujiokolea ,kabla ya kupanda chombo unatakiwa kuangalia kipo kwenye ubora unaostahili na kinaweza kukusaidia kwenye kusafiri kwenye mazingira salama.
“ Lakini jambo jingine ni namna bora ya kuvaa vifaa vya kujiokolea na kwanini lazima kuwepo na vifaa hivyo kwenye chombo kwani ndio sehemu ya uokozi kuwasaidia pale ajali zinazotokea”Alisema Captain Shalua
Akizungumzia kuhusu vifaa vya kuzimia moto,Captain Shalua alisema vifaa vya kuzimia moto vyombo vya majini vingi vinatumia mafuta ya petrol kwa hiyo wanapenda watumiaji wafahamu namna bora na kifaa gani sahihi cha kuzimia moto unaowaka na kusababishwa na mafuta.
“Kwani watu wengi wanakimbia maji na kiuhalisia huwawezi kuzima moto kwa namna hiyo bali ni vifaa maalumu poda na opovu ili kuweza kizima moto”Alisema
Awali akizungumza Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Amina Miruko alisema wataendelea kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na suala hilo
Alisema pia watahakikisha Bandari Bubu zilizopo kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini zinarasimishwa pale inapobidi na urasimishaji unaofanyika unakuwa rasmi ikiwemo kufanya kaguzi za kushtukiza na kupanga.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.