ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 3, 2020

WAFUNGWA 150 WAPELEKWA KWITANGA KULIMA MCHIKICHI

 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wapili kulia) na Mkuu wa Gereza Kwitanga, Mrakibu Mwandamizi, Dominick Kazmil wakiangalia matunda ya mchikichi yaliyovunwa katika gereza hilo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma  kuwa Kituo Kikuu cha  Uzalishaji wa zao la  Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa kufufua kilimo cha zao hilo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (watatu mstari wa mbele) akimsikiliza  Mkuu wa Gereza Kwitanga, Mrakibu Mwandamizi, Dominick   Kazmil baada ya kuangalia miche ya michikichi iliyooteshwa  katika gereza hilo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma  kuwa Kituo Kikuu cha  Uzalishaji wa zao la  Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa kufufua kilimo cha zao hilo.Wengine ni ujumbe uliofuatana na Naibu Waziri. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
 Matunda ya Mchikichi yaliyovunwa katika mashamba ya Gereza Kitwanga yakiwa yameanikwa juani tayari kwa kukamuliwa mafuta ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka Gereza hilo  lililopo wilayani Kigoma  kuwa Kituo Kikuu cha  Uzalishaji wa zao la  Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa kufufua kilimo cha zao hilo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiangalia mpango kazi wa kilimo cha mchikichi katika Gereza la Kwitanga ikiwa ni ufuatiliaji wa  utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka Gereza hilo  lililopo wilayani Kigoma  kuwa Kituo Kikuu cha  Uzalishaji wa zao la  Mchikichi nchini ikiwa ni mkakati maalumu wa kufufua kilimo cha zao hilo,Kushoto ni Mkuu wa Gereza  Mrakibu Mwandamizi, Dominick Kazmil na Kulia ni Mkuu wa Magereza Kigoma Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri. 
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Na Mwandishi Wetu,Kigoma

Wafungwa 150 kutoka katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora wamepelekwa katika Gereza la Kwitanga Mkoani Kigoma ikiwa ni mkakati maalumu wa Serikali kuliteua gereza hilo kuwa Kituo Kikuu cha Uzalishaji wa zao la  mchikichi nchini.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mkakati huo uliotolewa maagizo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katikati ya mwaka 2018 alipofanya ziara gerezani hapo  ukiwa na lengo la kulifanya Jeshi la Magereza kuingia katika mfumo wa uzalishaji mali.

“Katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambalo ni agizo la serikali, wizara tumeongeza nguvukazi hapa kwa kuleta wafungwa 150 na muda si mrefu tutaongeza wafungwa wengine 300 kutoka magereza mbalimbali nchini ili kuweza kuongeza uzalishaji huku eneo lenye ukubwa wa ekari 6000 linatarajiwa kulimwa zao hilo sambamba na kusambaza mbegu zinazozalishwa gerezani hapo kwenda Halmashauri za Mikoa, Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi,” alisema Masauni

“Lakini pia ili kuliwezesha gereza hili tumeliagiza Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza kulichukua Gereza la Kwitanga na kuliingiza katika kundi la magereza yanayowezeshwa na shirika ili kuweza kutatuliwa matatizo yao ya kifedha badala ya kusubiri bajeti kuu kutoka serikalini ambayo inakua haitoshi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Magereza mkoani Kigoma, Kamishna Msaidizi Leonard Bushiri aliunga mkono hoja ya Gereza Kwitanga kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali huku akikiri baadhi ya masuala kukwama kutokana na changamoto za kibajeti.

“Nafikiri hili suala la gereza kuchukuliwa na Shirika la Uzalishaji Mali litatatua changamoto nyingi za kibajeti na kiuendeshaji maana gereza halina gari kubwa kwa ajili ya uvunajina usafirishaji wa mafuta kutoka gerezani kwenda kwa mtumiaji, hakuna bajeti ya uendeshaji kwa mfano kukamua lita 100 mpaka 120 za mafuta tunahitaji maji lita 1000 hivyo fedha kwa ajili ya kununulia umeme ili kusukuma maji ni changamoto, kwahiyo kuingizwa kwenye shirika itasaidia changamoto nyingi” alisema ACP Bushiri

Sambamba na kulima zao la mchikichi Gereza Kwitanga linalima pia mahindi, mpunga, mihogo, maharage na Bustani za mbogamboga.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.