ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, April 5, 2019

RAIS MAGUFULI: HATUNA MPANGO WA KUONGEZA MIKOA MIPYA.

Na Mwandishi Wetu
MAELEZO
DAR ES SALAAM

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali haina mpango wa kuongeza maeneo ya utawala ikiwemo kuanzisha mikoa mipya na badala yake imejipanga kuimarisha huduma na mahitaji ya miundombinu iliyopo ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru yenye urefu wa kilometa 193 leo (Ijumaa April 5, 2019), Rais Magufuli alisema Serikali imekusudia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, maji, elimu n.k katika maeneo waliopo.
Aliongeza kuwa katika awamu yake yake ya Uongozi, suala la kuongeza maeneo ya utawala halipo na badala yake kuwataka Viongozi wa maeneo hayo wajipange katika kuwaletea maendeleo wananchi badala ya fedha zilizopo kwenda katika kujenga ofisi mpya za Wakuu wa Mikoa mipya na kuwalipa mishahara viongozi hao.
“Tumepanga kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wetu, tumechelewa kuleta Maendeleo hususani kwa wananchi wetu wa mikoa ya kusini, Serikali ninayoiongoza haina mpango wa kuanzisha mikoa mipya , badala yake pesa hizo tutazielekeza katika ununuzi wa madawa na kuboresha miundombinu ya barabara, elimu na nishati’ alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema bado yapo baadhi ya maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara za lami, hivyo Serikali haitoweza kuleta Maendeleo katika sehemu moja kwa kuwa fedha hizo hazipo kwa kuwa ina na mahitaji makubwa katika kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma muhimu na za msingi kwa Maendeleo ya wananchi zinapewa kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati, kwa kuwa kukamilika kwake kutasaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto ambavyo katika miaka ya nyuma vimekuwa vikisababisha vifo vya makundi hayo ya kijamii.
Akizumgumzia kuhusu Sekta ya Maji, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa kuwasimamia wakandarasi wa miradi ya maji nchini, kwani Serikali imekuwa ikitenga kiasi kikubwa cha cha fedha katika miradi ya Maendeleo pasipo na kupata matokeo yaliyotarajiwa, na hivyo kuisababishia hasara Serikali.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Fedha na Mipango, miradi mingi ya maji imekuwa ikitumia fedha nyingi pasipo na kupata matokeo yoyote na wataalamu wetu hasa wakandarasi wamekuwa wazito kutoa tafsiri za nadharia za utaalamu na kuzileta katika nadharia halisi, na mataifa ya nje yanashangwa tunaposhindwa kuvitumia vyanzo tulivyonazo ili kuweza kuzalisha maji ya kutosha’ alisema Rais Magufuli.
Awali akizungumzia kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema kujengwa kwa barabara hiyo kutaimarisha mawasiliano katika ukanda wa kusini unaojumuisha Mtwara, Mingoyo, Masasi, Mangaka, Tunduru hadi Mbamba Bay na hivyo kuzidi kufungua fursa za kiuchumi nanchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Alisema hadi kukamilika kwake barabara hiyo imegharimu kiasi cha Tsh Bilioni 173, ambapo Shirika la Misaada la Japan limetoa asilima 23.24, Benki ya Maendeleo ya Afrika asilimia63.32 na Serikali ya Tanzania asilimia 13.35 ikiwemo kodi na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Shinichi Goto alisema Serikali ya Japan imekuwa mstari wa mbele kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo barabara ya Namtumbo-Kilimasera-Matemanga-Tunduru na itaendelea kusaidia miradi mingine ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuondoa umaskini kwa wananchi wake yanafikiwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.