ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, August 15, 2018

JUMLA YA WANANCHI 2,587 WA KIJIJI CHA LUPEMBELWASENGA WAMEKABIDHIWA HATI MILIKI ZA KIMILA

  Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi  Angelina Mabula akikabidhi hati za kimira kwa wananchi wa kijiji cha Lupembelwasenga Wilaya ya Iringa Vijijini  mkoani Iringa
 Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi  Angelina Mabula  akiwa na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela,mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Ritta Kabati pamoja na viongozi wa LTA wakati wa ugawaji wa hati za kimila


NA FREDY MGUNDA IRINGA.

Wananchi 2,587 wa kijiji cha Lupembelwasenga Wilaya ya Iringa Vijijini wamekabidhiwa Hati za Hakimiliki ya Kimila chini ya Mradi wa LTA Uliofadhiliwa na wadau kutoka Marekani wa Feed the Future USAID.

Akizungumza wakati wa kukabidhi Hati hizo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi  Angelina Mabula alisema kuwa katika miaka miwili ya utekelezaji,Mradi huo umeweza kutoa jumla ya Hati za Hakimiliki ya Kimila 35,286 katika vijiji 26.
Mabula alisema kuwa hati hizo zitawasaidia kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa kuzingatia uwezo wa ardhi kuhimili idadi hiyo na kasi ya ongezeko la watu na mifugo kwa miaka mingi ijayo.

Mabula aliongezea kuwa,hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuimarisha usalama wa miliki za ardhi na kuongeza thamani ambayo itawawezesha hata kukopesheka katika taasisi za kifedha zikiwemo benki.

“Usajili wa ardhi ni muhimu kwasababu unaongeza ulinzi wa umiliki wa ardhi, unawezesha uwekezaji, unaongeza thamani ya ardhi na unapunguza migogoro ya ardhi,” alisema Mabula

Mabula aliupongeza mpango huo akisema utasaidia kupunguza eneo kubwa la ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambayo haijapimwa.

Aidha Mabula aliwaomba Feed The Future wautanue mradi huo angalau ufike umalize kupima vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa  huku akivikumbusha vijiji vyote vya wilaya hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kwenye miradi ambayo inasaidia kukuza maendeleo ya nchi. 

“Tunataka katika kipindi ambacho Mradi wa Urasimishaji Ardhi (LTA) unaofanywa chini ya mpango wa Feed The Future kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) tuhakikishe tunapima ardhi na mipango ya matumizi bora na ipimwe ili kila mwenye kipande chake cha ardhi awe na hati yake,” alisema Mabula.

Alisema kwa kupitia sera hiyo, kutakuwa na usimamizi zaidi wa ulinzi wa ardhi ya watu masikini ili kupunguza uporaji wa rasilimali hiyo unaofanywa na matajiri.

“Marekebisho ya sera hiyo ya ardhi yatawezesha pia kufanyika kwa mrekebisho ya sheria mbalimbali za ardhi ili ziendane na sera na mazingira ya sasa,” alisema Mabula.


Mabula aliwataka wanakijiji wa kijiji hicho ambao hawajapimiwa maeneo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo ubishi na migogoro ya kifamilia kutumia vizuri muda ambao bado mradi huo upo katika wilaya hiyo na kuhakikisha nao wananufaika na zoezi hilo.

Wanakijiji ambao hawajapimiwa maeneo yao wanaweza kuendeleoa kuzalisha migogoro ambayo haina tija kwa maendeleo yao na kusababisha waendelee kuwa masikini kwa kuwa hawatakuwa na dhamana ya kwenda kukopa
Mabula alimalizia kwa kuwataka wananchi wote waliopokea Haki hizo kutambua na kuheshimu wajibu wao kwa jamii na Taifa kwa ujumla katika matumizi na usimamizi mzuri wa Ardhi.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Mradi huo Ndugu Malaki Msigwa alisema kuwa mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kutoa Hati kwa usawa Wanawake na Wanaume.
Msigwa aliwapongeza wataalamu wa mradi huo kwa kuhakikisha wanawasaidia wananchi wa kijiji cha Lupembelwasenga kupima maeneo yao na kupata hati miliki za kimila ambazo zitakuwa msaada mkubwa kwenye maendeleo ya kiuchumi.

“Baadhi ya miradi imeibuliwa wakati wa upimaji wa ardhi hivyo ni fursa sasa kwa wananchi wenyewe kuitumia vizuri ardhi waliyopimiwa na kupewa hati miliki za kimila na kwa kuwa asilimia fulani kijiji hiki kimepimwa hivyo wanaweza kuwa kijiji cha mfano kwa kuwapa maendeleo hata wawekezaji wazuri kwa faida yao” alisema Msigwa

Msigwa alisema kati ya vijiji hivyo 41 vitakavyotayarishiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kila mwenye ardhi kupimiwa na kupewa hati miliki za kimila, vijiji 36 vipo wilayani Iringa na vitano vipo wilayani Mbeya.

“Baada ya kukamilisha zoezi la upimaji mashamba na urasimishaji wa kijiji chote cha Lupembelwasenga, hivi sasa mradi unaendelea na upimaji mashamba katika vijiji vya mradi ambavyo vipo wilayani Iringa” alisema Msigwa

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya aliupongeza Mradi wa Urasimishaji Ardhi (LTA) unaofanywa chini ya mpango wa Feed The Future kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa kuzingatia jinsia wakati walipokuwa wanaendesha zoezi la upimaji ardhi katika kijiji hicho.

“Hongera sana LTA kwa kuwapa elimu wanawake na wanaume na kuhakikisha kuwa wanapa haki zao sawa bila kuwa na mgogoro wowote tofauti na ilivyokuwa hapo awali,maana miaka ya nyuma mwanamke alikuwa anabaguliwa kwenye kila kitu wala alikuwa haruhusiwi hata kumili ardhi” alisema Masunya
Masunya aliongeza kwa kusema kuwa wanakijiji wa kijiji cha Mlanda baada ya kupata elimu ya kumiliki ardhi kumepunguza sana migogoro ambayo ilikuwa inaleta chuki kwenye familia.

“Kwa sasa ardhi ya kijiji hiki imepanda dhamani kwa kiasi kikubwa na tayari ishapimwa na mmepata hati miliki za kimila ambazo zitawasaidia katika maendeleo yenu ya kiuchumi” alisema Masunya

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Lupembelwasenga Mshauri wa Kijiji Ndugu Titus Maketta ameshukuru Msaada wa Marekani uliofadhili Mradi wa urasimishaji wa Ardhi LTA kwa kuwawezesha kupata Hati za Hakimiliki za kimila zitakazowaondolea migogoro ya Ardhi.
Zoezi la ugawaji wa Hati za Hakimiliki ya Kimila Kijiji cha Lupembelwasenga umeambatana na Naibu waziri Mhe. ANGELINA MABULA kufungua Masjala ya Ardhi Kijijini hapo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.