Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kumewezesha kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakitamba kwamba hawawezi kuguswa na kupelekea wengine kukimbia nchi.
Waziri Majaliwa amesema hayo leo wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yaliyofanyika uwanja wa Gangilonga, mkoani Iringa.
"Sasa hivi dawa zinakamatwa kwelikweli na wale wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokuwa wakijiita vigogo na kutamba kuwa hawakamatwi na hata wakikamatwa wanaachiwa, wameanza kuikimbia nchi. Nawasihi viongozi wa siasa, dini pamoja na vyombo vya habari, tuendelee kukemea kwa nguvu zote matumizi na biashara ya dawa za kulevya", amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali baada ya kuanzisha Mamlaka hiyo, iliiwezesha kwa kuipatia rasilimali fedha, watendaji na vitendea kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amesema matumizi ya dawa za kulevya yapo zaidi kwenye miji mikubwa hasa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga na Mwanza, pia kasi ya kuenea kwa matumizi hayo kwenye miji midogo nayo ni kubwa hasa katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Mbeya na Morogoro.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.